Michezo

Messi afikia rekodi ya Pele kwa kufunga mabao 643 akichezea klabu moja

December 20th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifikia rekodi ya nguli wa soka nchini Brazil, Pele, ya kufungia klabu moja jumla ya mabao 643 baada ya kucheka na nyavu za Valencia katika sare 2-2 iliyosajiliwa na Barcelona katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Disemba 19, 2020.

Messi, 33, alifikia rekodi hiyo alipofunga kwa kichwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza, dakika chache baada ya penalti yake kupanguliwa na kipa Jaume Domenech.

Bao la kwanza kwa Messi ambaye ni raia wa Argentina kufungia Barcelona ni mnamo 2005 dhidi ya Albacete.

Katika enzi zake za usogora, Pele alipachika wavuni jumla ya mabao 643 katika kipindi cha misimu 19 akichezea kikosi cha Santos nchini Brazil kati ya 1956 na 1974.

Hata hivyo, raha ya mafanikio ya Messi iliyeyushwa na tukio la Barcelona kushindwa kuwapiga Valencia ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 12 kwa alama 15 sawa na Eibar.

Barcelona ambao ni mabingwa mara 26 wa La Liga wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 21, nane zaidi nyuma ya viongozi Atletico Madrid waliowapokeza Elche kichapo cha 3-1 katika mechi nyingine ya Jumamosi.

Real Madrid ambao ni washindani wakuu wa Barcelona kwenye La Liga, wanajivunia alama tatu zaidi kuliko Barcelona japo wana mchuano mmoja zaidi kusakata dhidi ya Eibar mnamo Disemba 20 ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na Barcelona.

Licha ya beki Mouctar Diakhaby kuwaweka Valencia uongozini katika dakika ya 29, Barcelona walirejea mchezoni kupitia bao la Messi kabla ya Ronald Araujo kufunga la pili kwa upande wa masogora wa kocha Ronald Koeman.

Ingawa hivyo, utepetevu wa mabeki wa Barcelona uliruhusu Valencia kusawazishiwa na Maxi Gomez katika dakika ya 69.

Gomez ambaye ni raia wa Uruguay, sasa amehusika katika mabao mawili kati ya sita ambayo Valencia wamefunga ligini kutokana na mechi saba zilizopita dhidi ya Barcelona.

Mbali na Messi na Antoine Griezmann, nyota mwingine wa Barcelona ambaye alipoteza nafasi nyingi za wazi dhidi ya Valencia ni kiungo wa zamani wa Liverpool na Bayern Munich, Philippe Coutinho aliyepaisha mpira katika dakika ya 78 licha ya kusalia peke yake na kipa Domenech.