Messi afunga mawili dhidi ya Bilbao na kubeba Barcelona hadi tatu-bora La Liga

Messi afunga mawili dhidi ya Bilbao na kubeba Barcelona hadi tatu-bora La Liga

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga mabao mawili na kuongoza Barcelona kupaa hadi nafasi ya tatu jedwalini baada ya kuwatandika Athletic Bilbao 3-2 kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Januari 6, 2020.

Bilbao waliokuwa wakichezea nyumbani waliwekwa kifua mbele na Inaki Williams katika dakika ya tatu kabla ya chipukizi Pedri Gonzalez kusawazisha mambo kupitia mpira wa kichwa kunako dakika ya 14.

Messi aliyeshuhudia makombora yake mawili yakibusu mhimili wa lango la Bilbao, aliwarejesha Barcelona uongozini katika dakika ya 38 kabla ya kufunga goli la tatu dakika 24 baadaye. Mabao yote mawili ya Messi yalichangiwa na Pedri aliyemtatiza pakubwa kipa Unai Simon wa Bilbao.

Goli la Iker Muniain katika dakika ya 90 kwa upande wa Bilbao halikutosha kuyumbisha safu ya nyuma ya Barcelona iliyosalia imara hadi kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Ushindi wa Barcelona uliwashuhudia wakichupa hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 31, tano nyuma ya mabingwa watetezi Real Madrid ambao ni wa pili kwenye msimamo wa jedwali linaloongozwa na Atletico Madrid kwa pointi 38. Real Sociedad ambao wamecheza mechi 18, mojaz zaidi kuliko Barcelona na Real wanafunga mduara wa nne-bora kwa alama 30.

Nafuu zaidi kwa Atletico wanaotiwa makali na kocha Diego Simeone ni kwamba wana michuano miwili zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na washindani wao wakuu – Real na Barcelona.

You can share this post!

Miamba Atletico Madrid watolewa mapema kwenye kivumbi cha...

Hofu Lamu kufuatia ongezeko la vijana wanaotumia dawa za...