Michezo

Messi afunga penalti ya kwanza msimu huu

September 30th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga penalti na kumsaidia kocha Ronald Koeman kuanza vyema ukufunzi wake kambini mwa Barcelona kwa ushindi wa 4-0 dhidi ya Villarreal katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Chipukizi Ansu Fati ndiye aliibuka mchezaji bora wa gozi hilo baada ya kupachika wavuni mabao mawili baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi alizopokezwa na Jordi Alba na Philippe Coutinho katika dakika za 15 na 19 mtawalia.

Fati, 17, pia alichangia penalti iliyofumwa wavuni na Messi kunako dakika ya 35.

Barcelona walifunga karamu yao ya ufungaji mabao katika dakika ya 45 baada ya Pau Torres kujifunga baada ya kubabatiza na mpira ulioelekeza langoni na Messi.

Chini ya kocha Unai Emery, Villarreal walizidiwa maarifa katika takriban kila idara na jaribio lao la pekee langoni pa Barcelona lilitokea mwishoni mwa kipindi cha pili.

Messi ndiye mwanasoka wa sita kufunga bao katika kila mchuano wa mwanzo wa misimu wa La Liga kwa miaka 17 iliyopita. Anaungana sasa na beki na nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos aliyewaongoza waajiri wake kupepeta Real Betis 3-2 mnamo Septemba 26.

Mechi dhidi ya Villarreal ilikuwa ya kwanza kwa Messi kuchezea Barcelona katika La Liga tangu ajaribu kuagana na kikosi hicho mwishoni mwa msimu uliopita.

Messi, 33, aliwawasilishia Barcelona ombi la kutaka kubanduka ugani Camp Nou ila uhamisho wake hadi Manchester City ya Uingereza ukagonga ukuta baada ya mnunuzi wake kutakiwa kuweka mezani kima cha Sh89 bilioni.

Messi aliyelenga shabaha langoni pa Villarreal mara saba, alimfanyisha kipa Sergio Asenjo kazi ya ziada mwishoni mwa kipindi cha pili.

Koeman aliaminiwa fursa ya kuwa mrithi wa Quique Setien aliyetimuliwa baada ya Barcelona kudhalilishwa 8-2 na Bayern Munich kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uliopita.

Coutinho, aliyewafungia Bayern mabao mawili katika mechi hiyo ya UEFA, alirejea Barcelona msimu huu baada ya kipindi chake cha mkopo kukamilika rasmi uwanjani Allianz Arena.

Miralem Pjanic, Francisco Trincao na Pedri Lopez waliosajiliwa na Barcelona muhula huu, pia waliunga kikosi cha kwanza cha kocha Koeman.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO