Michezo

Messi aibuka mchezaji bora kwa mara ya sita

December 4th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

LIONEL Messi wa klabu ya Barcelona ndiye mshindi wa Ballon d’Or kwa mwaka huu wa 2019, hii ikiwa mara yake ya sita.

Raia huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 32 alitwaa tuzo hiyo baada ya kuikosa tangu 2015.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na beki Virgil van Dijk raia wa Uholanzi, akiwa mchezaji wa nne wa Liverpool katika saba bora, akiwemo mshambuliaji Sadio Mane aliyemaliza katika nafasi ya nne, huku Mohammed Salah akifunga ukurasa wa tano bora.

Staa Cristiano Ronaldo raia wa Ureno anayechezea klabu ya Juventus nchini Italia alimaliza wa tatu, baada ya kutunukiwa tuzo hiyo mara tano hapo awali.

Messi na Ronaldo wamekuwa wakibadilishana tuzo hiyo tangu 2008, wote wakiwa washambuliaji matata, ambao kufikia 2017 kila mmoja alikuwa ameshinda mara tano.

Kiungo mahiri wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric alipenya na kutwaa tuzo hiyo mwaka 2018.

Baada ya kumpiku Ronaldo, Messi amekuwa mchezaji wa kwanza kubeba tuzo hiyo mara sita.

Ilikuwa mara ya tatu kwa mwaka 2019 kwa Messi, Ronaldo na Van Dijk kuwania tuzo moja kwa pamoja.

Mara ya kwanza ilikuwa wakati tuzo ya Mchezaji Bora barani Ulaya la UEFA mwezi Agosti ambapo Van Dijk aliibuka mshindi.

Mara ya pili waliwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (Fifa) ambapo Messi alishinda.

Tuzo ya Ballon d’Or imekuwa ikipiganiwa kila mwaka tangu 1956 ambapo mshindi wa kwanza mwaka huo alikuwa Stanley Mathews wa Uingereza.

Awali, tuzo hiyo ilikuwa ikiwaniwa tu na wachezaji wa Ulaya kabla ya kufanyika mabadiliko mnamo 1995 na kujumuisha wachezaji wa mataifa yote duniani, mradi wawe wasakataji soka barani Ulaya.

Orodha ya majina ya wachezaji 30 bora hutangazwa na baadaye kupigiwa kura na waandishi wa habari za michezo kutoka sehemu tofauti duniani, ambapo kila nchi hupiga kura moja.

Kuanzia 2010 hadi 2015, tuzo hiyo iliunganishwa na ile ya Fifa lakini zilitengana mnamo 2016 ambapo Fifa ilianza kuandaa tuzo zao wenyewe.

Ronaldo alitwaa tuzo ya 2008 akifuatiwa na Lionel Messi huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Fernando Torres.

Mshindi wa 2009 alikuwa Messi akifautiwa na Ronaldo halafu Xavi. 2010: Messi, Andres Iniesta na Xavi. 2011: Messi, Ronaldo, Xavi. 2012: Messi, Ronaldo, Iniesta. 2013: Ronaldo, Messi, Frank Ribery. 2014: Ronaldo, Messi, Manuel Neuer. 2015: Messi, Ronaldo, Neymar. 2016 Ronaldo, Messi, Antoine Griezmann. 2017 Ronaldo, Messi, Neymar. 2018: Luka Modric, Ronaldo, Griezmann. 2019: Messi, Virgil van Dijk, Ronaldo.