Michezo

Messi aishauri Barca iwauze Coutinho, Rakitic na Umtiti

May 13th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

NYOTA wa Barcelona Lionel Messi anadaiwa kueleza uongozi wa timu hiyo kuwatimua Philippe Coutinho, Ivan Rakitic na Samuel Umtiti akisema fomu yao imedorora na hawafai kuichezea klabu hiyo tena.

Ingawa Barcelona tayari imeshinda taji la La Liga msimu huu wa 2018/19 ukiendela kukamilika, walijipata pabaya kwa mara nyingine kwenye kipute cha Klabu Bingwa Barani Uropa (UEFA) kwa kubanduliwa na Liverpool inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Barcelona walitolewa kwenye UEFA licha ya kutwaa ushindi wa 3-0 katika mkondo wa kwanza uliosakatwa ugani Camp Nou ila kichapo cha 4-0 walichopokezwa ugani Anfield kikawaondoa kwenye kiny’ang’anyiro hicho.

Mabingwa hao watetezi wa Laliga walijipata katika hali sawa na hiyo msimu wa 2017/18 walipopoteza uongozi wa 4-1 dhidi ya Roma na kuishia kuchapwa 3-0 nchini Italia.

Kulingana na jarida la Daily Star, Messi ameueleza uongozi wa Barcelona kuwatimua Continho, Rakitic na Umtiti ili kuwasajili wachezaji wapya watakaoongeza nguvu kwenye safu za kiungo na ushambulizi za Barcelona.

Countinho aliyejiunga na Barcelona kutoka Liverpool Januari 2018, amekuwa na msimu mgumu Uhispania na amekuwa akipangwa katika kikosi cha kwanza na kocha Ernesto Valverde wakati Ousmane Dembele anauguza jeraha.

Rakitic na Umtiti nao wamekuwa na fomu isiyoridhisha na iwapo matakwa ya Messi yatazingatiwa basi shoka la kuwaondoa Barcelona huenda likawaangukia.