Michezo

Messi alilipwa Sh13.7 bilioni msimu uliopita

September 15th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi ndiye mwanasoka anayedumishwa kwa mshahara wa juu zaidi duniani kufikia sasa mwaka huu. Haya ni kwa mujibu wa kampuni ya Forbes ambayo imekadiria kwamba Messi alilipwa kima cha Sh13.7 bilioni katika mwaka wa 2019-20.

Cristiano Ronaldo wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno ndiye wa pili katika orodha hiyo baada ya kutia kapuni jumla ya Sh12.6 bilioni katika msimu uliopita wa 2019-20.

Neymar wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Brazil ndiye wa tatu akifuatiwa na Kylian Mbappe wa PSG na timu ya taifa ya Ufaransa.

Wanasoka watatu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) – Mohamed Salah, Paul Pogba na David Pogba ndio wanakamilisha orodha hiyo ya 10-bora iliyojumuisha pia mwanasoka matata wa Real Madrid na timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale.

Bale aliorodheshwa katika nafasi ya nane baada ya kupokezwa jumla ya Sh3.1 bilioni licha ya kutojivunia msimu wa kuridhisha katika mwaka wa 2019-20 baada ya uhusiano wake na kocha Zinedine Zidane kuvurugika. Bale aliwajibishwa katika mechi mbili pekee kati ya 14 za mwisho zilizosakatwa na waajiri wake Real katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Salah wa Liverpool aliibuka katika nafasi ya tano, mbele ya Pogba wa Man-United aliyeshikilia nafasi ya sita huku

Fowadi Antoine Griezmann wa Barcelona aliorodheshwa katika nafasi ya saba huku mshambuliaji matata wa Bayern Munich, Robert Lewandowski akiridhika katika nafasi ya tisa.

Nafasi tatu za kwanza kwenye orodha hiyo ilisalia jinsi ilivyokuwa mnamo 2019 ingawa Mbappe alipanda juu kwa nafasi tatu zaidi kutoka nafasi ya saba mnamo 2018-19 hadi nafasi ya nne msimu huu wa 2019-20.

Messi, 33, aliwasilisha ombi la kuagana na Barcelona mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 ila Manchester City waliokuwa wakimvizia wakashindwa kuweka mezani Sh89 bilioni za kushawishi waajiri wake kumwachilia.

ORODHA YA WANASOKA WANAOPOKEA UJIRA WA JUU ZAIDI DUNIANI:

1 Lionel Messi (Barcelona na Argentina) Sh13.6 bilioni

2 Cristiano Ronaldo (Juventus na Ureno) Sh12.6 bilioni

3 Neymar (Paris St-Germain na Brazil) Sh10.4 bilioni

4 Kylian Mbappe (Paris St-Germain na Ufaransa) Sh4.5 bilioni

5 Mohamed Salah (Liverpool na Misri) Sh3.9 bilioni

6 Paul Pogba (Manchester United na Ufaransa) Sh3.7 bilioni

7 Antoine Griezmann (Barcelona na Ufaransa) Sh3.6 bilioni

8 Gareth Bale (Real Madrid na Wales) Sh3.1 bilioni

9 Robert Lewandowski (Bayern Munich na Poland) Sh3 bilioni

10 David de Gea (Manchester United na Uhispania) Sh2.9 bilioni

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO