Michezo

Messi amtunuka marehemu Maradona bao lake kwenye mechi ya Barcelona dhidi ya Osasuna

November 30th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alitumia mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) uliowakutanisha waajiri wake Barcelona na Osasuna kumwomboleza aliyekuwa nguli wa soka nchini Argentina, Diego Maradona.

Messi, 33, alifunga bao la nne la Barcelona katika ushindi wa 4-0 waliousajili katika mchuano huo mnamo Novemba 29, 2020, uwanjani Camp Nou, Barcelona.

Fowadi huyo raia wa Aregentina alivua jezi yake ya Barcelona na kusalia na ile ya kikosi cha Newell Old Boys kilichowahi kumpa hifadhi Maradona katika enzi yake ya usogora mnamo 1993.

Baada ya kufunga bao na kuvua jezi ya Barcelona, Messi alitazama runinga kubwa iliyokuwa ikionyesha picha ya Maradona uwanjani Camp Nou na kuinua mikono yake yote miwili hewani.

Martin Braithwwaite, Antoine Griezmann na Philippe Coutinho walifunga mabao mengine ya Barcelona katika mchuano huo.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Barcelona walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo dhidi ya Osasuna wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kushinda mara moja pekee kutokana na michuano sita ya awali ya La Liga.

Maradona ambaye ni miongoni mwa wanasoka bora zaidi wa muda wote duniani, aliaga dunia mnamo Novemba 25, 2020 akiwa na umri wa miaka 60.

Messi aliwahi pia kuchezea kikosi cha Newell Old Boys jijini Rosario, Argentina kabla ya kujiunga rasmi na Barcelona.

Maradona aliwahi pia kusakatia Barcelona kati ya 1982 na 1984, kabla ya kujiunga na Napoli ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).