Messi apewa kadi nyekundu ya kwanza akichezea Barca

Messi apewa kadi nyekundu ya kwanza akichezea Barca

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi, 33, alionyeshwa kadi nyekundu kwa mara ya kwanza akiwa mchezaji wa Barcelona katika fainali ya Spanish Super Cup iliyoshuhudia Athletic Bilbao wakisajili ushindi wa 3-2 jijini Seville mnamo Jumapili.

Messi aliyekuwa akiwajibishwa na Barcelona kwa mara ya 753, alimkabili visivyo kiungo Asier Villalibre na tukio hilo la dakika ya 120 likathibitishwa na teknolojia ya VAR.

Ingawa Barcelona walijipata uongozini mara mbili kupitia mabao ya Antoine Griezmann, juhudi zao zilifutwa na Oscar de Marcos na Villalibre kabla ya Inaki Williams kufungia Bilbao bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ufanisi huo ulivunia Bilbao taji lao la pili tangu 1985.

Hadi kufikia Jumapili, Messi alikuwa amefurushwa uwanjani kwa kuonyeshwa kadi nyekundu mara mbili pekee akivalia jezi za timu ya taifa ya Argentina.

Mara ya kwanza ilikuwa katika mchuano wake wa kwanza kambini mwa Argentina mnamo 2005 dhidi ya Hungary kisha kwenye mechi ya kutafuta mshindi nambari tatu na nne katika fainali za Copa America mnamo 2019 dhidi ya Chile.

Adhabu ambayo Messi alipokezwa dhidi ya Bilbao huenda inatarajiwa sasa kumweka nje ya mechi nne zijazo za kuwania mataji mengine isipokuwa ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Ushindi kwa Barcelona katika mchuano huo ungaliwavunia taji lao la 14 la Super Cup na la kwanza kwa kocha mpya Ronald Koeman. Aidha, Messi angalitia kapuni taji lake la nane la Super Cup kambini mwa Barcelona katika msimu wake wa mwisho wa usogora uwanjani Camp Nou.

Bilbao ambao walipepeta Real Madrid 2-1 kwenye nusu-fainali, sasa wamepiga Real na Barcelona katika mechi mbili mfululizo kwa mara ya kwanza tangu 1960.

Barcelona walifuzu kwa fainali ya Super Cup msimu huu baada ya kuwazidi ujanja Real Sociedad kupitia mikwaju ya penalti. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa miamba hao kupigwa baada ya mechi 10 na kichapo hicho kilitamatisha rekodi ya Messi aliyejikuwa akijivunia mabao manne kutokana na mechi mbili na magoli sita kutokana na michuano mitano ya awali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uhuru hawezi kunisaliti – Raila

Wanafunzi wa elimu ya msingi waanza mitihani ya majaribio