Michezo

Messi ashindwa kuisaidia Barca UEFA

April 11th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MCHEZAJI matata wa Barcelona Lionel Messi Jumanne usiku alishindwa kuisaidia timu yake kuona mlango wa nusu fainali ya UEFA Klabu Bingwa Ulaya timu hiyo ilipolemewa kufunga bao hata moja ugenini dhidi ya AS Roma.

Roma iligeuza ubao kwa namna mbayo hakuna aliyetarajia, hasa dhidi ya miamba ambao wana uzoefu wa kipute hicho.

Ingawa mdahalo mkuu ulikuwa kuhusu ikiwa Man City ingetumia fursa ya nyumbani kuibandua Liverpool, hakuna aliyekuwa na matumaini kuwa Roma ingeitoa Barcelona nyama mdomoni na kuilazimisha kusahau nusu fainali.

Licha ya kuwa na wachezaji wenzake wazoefu kama Jordi Alba, Sergio Busquets, Luis Suarez na Andres Iniesta, Messi alishindwa kuonyesha makali yake mbele ya goli.

Kabla ya mechi hiyo, Barcelona haikuwa imepoteza mechi yoyote Ulaya na La Liga. Lakini kulikuwa na tashwishi kabla ya mechi hiyo maanake Barca ilisaidiwa  na magoli mawili ya kujifunga ilipolima Roma 4-1 Camp Nou, hali iliyowahadaa Messi na wenzake kuwa mechi ya mardudiano ingekuwa rahisi.

Roma ilicheza mchezo wa kuridhisha Uhisapnia mechi ya mwanzo, lakini matokeo yao yalikuwa kama adhabu kwani ilikuwa wazi kuwa walikuwa wameondolewa kwenye kipute hicho.