Michezo

Messi atokea benchi na kuongoza Barcelona kusajili ushindi wa kwanza baada ya mechi tano za La Liga

November 8th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alitokea benchi mwanzoni mwa kipindi cha pili na kufunga mabao mawili yaliyosaidia Barcelona kupepeta Real Betis 5-2 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Novemba 7, 2020.

Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Barcelona kusajili baada ya mechi tano za La Liga.

Ousmane Dembele aliwaweka Barcelona uongozini kunako dakika ya 22 kabla ya fowadi Antoine Griezmann kupoteza mkwaju wa penalti.

Tukio hilo liliwapa Betis motisha zaidi na wakasawazishiwa na Antonio Sanabria sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

Messi alitokea benchi na kuchangia bao lililofungwa na Griezmann katika dakika ya 49 kabla ya nyota huyo raia wa Argentina kutikisa nyavu za Betis mara mbili kunako dakika za 61 na 82.

Licha ya beki Aissa Mandi kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kunawa mpira alioelekezewa na Dembele, Betis walipania kurejea mchezoni kupitia bao la Lorenzo Moron katika dakika ya 73. Hata hivyo, juhudi zao zilizimwa na chipukizi Pedri Gonzalez aliyefunga bao la tano la Barcelona katika dakika ya 90.

Bao la pili la Messi katika mechi hiyo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na beki Sergi Roberto. Hilo lilikuwa bao lake la kwanza katika ngazi ya klabu na kiwango cha timu ya taifa ambalo halikutokana na penalti.

Ushindi wa Barcelona ni nafuu tele kwa kocha Ronald Koeman ambaye hadi kufikia Novemba 7, 2020, alikuwa amewaongoza waajiri wake kujizolea alama mbili pekee kutokana na mechi nne za La Liga.

Barcelona kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama 11 sawa na Getafe na Elche. Ni pengo la pointi moja pekee ndilo linalowatenganisha Barcelona na Betis wanaoshikilia nafasi ya saba kwa alama 12.