Michezo

Messi awapokeza Barcelona barua ya kutaka wamwachilie aondoke ugani Camp Nou

August 26th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

LIONEL Messi amewataka waajiri wake Barcelona kumwachilia ajiengue ugani Camp Nou ili asake hifadhi mpya kwingineko muhula huu wa uhamisho.

Nyota huyo mzawa wa Argentina, 33, ametumia Barcelona barua ya faksi akieleza kwamba angependa kifungu kwenye kandarasi yake kinachompa idhini ya kuagana na miamba hao wa soka ya Uhispania bila ada yoyote kitekelezwe haraka iwezekanavyo.

Mbali na migogoro ya mara kwa mara kati ya wachezaji, usimamizi na benchi ya kiufundi kambini mwa Barcelona, kiini cha Messi kutaka kuagana na waajiri wake ni kichapo kinono cha 8-2 walichopokezwa na Bayern Munich ya Ujerumani kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu mnamo Agosti 16, 2020.

Aidha, matokeo duni ya Barcelona msimu huu yalishuhudia kikosi hicho kikikosa kutia kapuni taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2013-14. Hii ni baada ya kuambulia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na kubanduliwa mapema na Athletic Bilbao kwenye kivumbi cha Copa del Rey.

Messi, ambaye ni mshindi mara sita wa taji la Ballon d’Or ambalo mchezaji bora zaidi duniani hupokezwa, aliwajibishwa na Barcelona kwa mara ya kwanza mnamo 2004 na amewaongoza miamba hao kunyanyua ubingwa wa UEFA mara nne.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13 pekee, amefungia waajiri wake jumla ya mabao 634 kutokana na mechi 730 zilizopita na ndiye mwanasoka anayejivunia historia ya mafanikio makubwa zaidi ugani Camp Nou. Akisalia na mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake na Barcelona, Messi amenyanyulia kikosi hicho jumla ya mataji 33.

Licha ya Messi kutaka kuondoka ugani Camp Nou, Barcelona wamesisitiza kwamba kipengele au kifungu anachotaka Messi kutumia ili kuagana nao kilipitwa na wakati na kwa hivyo anasalia kuwa mchezaji wao hadi mwishoni mwa mwaka wa 2021.

Kwa mujibu wa Barcelona, yeyote anayetaka kumsajili Messi kwa sasa atalazimika kuweka mezani kima cha Sh78 bilioni ili kuwashawishi kumwachilia.

Bodi ya usimamizi wa Barcelona unatazamiwa kuandaa kikao cha dharura na kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, cha pekee ambacho kinaweza kumfanya Messi kubadilisha mawazo na kuendelea kuvalia jezi za waajiri wake wa sasa ni kujiuzulu kwa Rais Josep Maria Bartomeu.

Hata hivyo, vyombo vingi vya habari nchini Argentina na Brazil vimefichua kwamba vyanzo vya karibu na Messi vimeshikilia kuwa nyota huyo tayari ameamua kuondoka Camp Nou hata kama uchaguzi mpya wa Barcelona utaandaliwa haraka iwezekanavyo.

“Hatujawahi kumwona hapo zamani akiwa na ari kubwa ya kuondoka jinsi ilivyo kwa sasa,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Makabiliano ya kisheria sasa yanatazamiwa kuanza kati ya Barcelona na Messi ambaye katika mkataba wake, ana kifungu kinachomkubalia kubanduka ugani Camp Nou bila ada yoyote iwapo angewaarifu waajiri wake kuhusu matamanio hayo kabla ya Juni 10, 2020.

Hata hivyo, Barcelona imeshikilia kwamba tarehe hiyo ilishapita na kifungu hicho ambacho Messi anarejelea hakina mashiko. Mawakili wa Messi wanahisi kwamba kipindi hicho (cha hadi Juni 10) kinastahili kurefushwa hasa ikizingatiwa kwamba msimu huu wa 2019-20 wa La Liga ulirefushwa pia kwa miezi miwili hadi Agosti 2020 kutokana na janga la corona.

Matokeo duni ya Barcelona msimu huu yalichochea usimamizi wa kikosi hicho kumtimua kocha Quique Setien mnamo Agosti 18 na nafasi yake kutwaliwa na mkufunzi Ronald Koeman, 57.

Koeman alisajiliwa na Barcelona kwa miaka miwili baada ya kushawishiwa kuagana na timu ya taifa ya Uholanzi wakati akisalia na miaka miwili kwenye mkataba wake na kikosi hicho.

Katika enzi zake za usogora, Koeman aliwahi kuchezea Barcelona kati ya 1989 na 1995 na akawasaidia kunyanyua mataji manne ya La Liga na moja la UEFA.

Barcelona pia walimteua Ramon Planes kuwa mkurugenzi mpya wa kiufundi kambini mwao. Planes alikuwa msaidizi wa Eric Abidal aliyetimuliwa na Barcelona akiwa mkurugenzi wa spoti.

Kati ya vikosi ambavyo kwa sasa vinahusishwa na uwezekano mkubwa wa kumsajili Messi ni Manchester City, Inter Milan, Juventus na Paris Saint-Germain (PSG).