Messi aweka rekodi ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or kwa mara ya saba

Messi aweka rekodi ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or kwa mara ya saba

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, ameweka rekodi ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or ambayo hutolewa kwa Mchezaji Bora Duniani kwa mara ya saba.

Hafla ya kutawazwa kwa washindi wa mwaka huu iliandaliwa Jumatatu usiku katika ukumbi wa Theatre du Chatelet jijini Paris, Ufaransa.

Messi, 34, alisaidia Argentina kutia kapuni ubingwa wa Copa America. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kutwaa taji la haiba kubwa kimataifa akivalia jezi za kikosi hicho. Isitoshe, Messi alifunga mabao 40 mnamo 2021 – 28 akiwa Barcelona, manne akichezea PSG na manane akisakatia Argentina.

Robert Lewandowski wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Poland aliambulia nafasi ya pili, mbele ya Jorginho ambaye ni kiungo wa Chelsea na timu ya taifa ya Italia. Mshambuliaji Karim Benzema wa Real Madrid na Ufaransa alifunga orodha ya nne-bora kwenye tuzo hiyo.

Washindi wa Ballon d’Or hupigiwa kura na wanahabari 180 kutoka kote duniani. Tuzo hiyo haikutolewa mwaka wa 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Messi na Cristiano Ronaldo anayejivunia ushindi mara tano walitamalaki tuzo hiyo kati ya 2008 na 2019. Ilikuwa mnamo 2018 pekee ambapo mshindi alikuwa tofauti baada ya Luka Modric wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia kutawazwa mfalme. Messi aliibuka mshindi wa Ballon d’Or kwa mara nyingine mnamo 2009, 2010, 2011, 2012, 2015 na 2019.

Lewandowski alipachika wavuni mabao 53 kutokana na mashindano yote aliyochezea Bayern mnamo 2021 na akatuzwa taji la Mfungaji Bora wa Mwaka.

Orodha ya tuzo ya Ballon d’Or:

1. Lionel Messi (Paris St-Germain/Argentina, fowadi)

2. Robert Lewandowski (Bayern Munich/Poland, fowadi)

3. Jorginho (Chelsea/Italia, kiungo)

4. Karim Benzema (Real Madrid/Ufaransa, fowadi)

5. N’Golo Kante (Chelsea/Ufaransa, kiungo)

6. Cristiano Ronaldo (Manchester United/Ureno, fowadi)

7. Mohamed Salah (Liverpool/Misri, fowadi)

8. Kevin de Bruyne (Manchester City/Ubelgiji, kiungo)

9. Kylian Mbappe (Paris St-Germain/Ufaransa, fowadi)

10. Gianluigi Donnarumma (Paris St-Germain/Italia, kipa)

11. Erling Braut Haaland (Borussia Dortmund/Norway, fowadi)

12. Romelu Lukaku (Chelsea/Ubelgiji, fowadi)

13. Giorgio Chiellini (Juventus/Italia, beki)

14. Leonardo Bonucci (Juventus/Italia, beki)

15. Raheem Sterling (Manchester City/Uingereza, fowadi)

16. Neymar (Paris St-Germain/Brazil, fowadi)

17. Luis Suarez (Atletico Madrid/Uruguay, fowadi)

18. Simon Kjaer (AC Milan/Denmark, beki)

19. Mason Mount (Chelsea/Uingereza, kiungo)

20. Riyad Mahrez (Manchester City/Algeria, fowadi)

21. Bruno Fernandes (Manchester United/Ureno, kiungo), alishikilia nafasi moja na Lautauro Martinez (Inter Milan/Argentina, fowadi)

22. –

23. Harry Kane (Tottenham/Uingereza, fowadi)

24. Pedri (Barcelona/Uhispania, kiungo)

25. Phil Foden (Manchester City/Uingereza, fowadi)

26. Nicolo Barella (Inter Milan/Italia, kiungo), alishikilia nafasi moja na Ruben Dias (Manchester City/Ureno, beki) pamoja na Gerard Moreno (Villarreal/Uhispania, fowadi)

27. –

28. –

29. Luka Modric (Real Madrid/Croatia, kiungo), alishikilia nafasi moja na Cesar Azpilicueta (Chelsea/Uhispania, beki)

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Agizo kuhusu chanjo ya Covid-19 litaathiri uchumi...

Askofu Ole Sapit asimama imara kuzima siasa kanisani

T L