Michezo

Messi hunirahisishia kazi uwanjani – Dembele

February 18th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

WINGA wa Barcelona Ousmane Dembele amesifu ushirikiano wake na nyota wa timu hiyo Lionel Messi akisema umemsaidia sana kuimarisha mchezo wake msimu huu.

Dembele ambaye yupo katika msimu wake wa pili Barcelona alimtaja Messi kama mchezaji bora duniani na kusema ushirikiano wao tayari umewazalishia mabao 43 msimu huu.

Mwanasoko huyo raia wa Ufaransa alikuwa akisakatia Borussia Dortmund kabla ya kutua Barcelona kurithi nafasi ya Neymar aliyehamia PSG ya Ufaransa ili kupunguza ushindani kati yake na Messi timuni.

“Messi hufanya kucheza soka iwe rahisi. Mimi humpokeza mipira kisha yeye huyafunga mabao. Akiwa uwanjani mambo huwa rahisi mno kwasababu kila mchezaji wa timu pinzani humwangazia na kuwaacha wachezaji wengine kutamba,” akasema Dembele.

Wachezaji hao wawili watakuwa na ushawishi mkubwa Barca watakapocheza na Lyon ya Ufaransa ugenini Jumanne Februari 19, 2019 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya kufuzu robo fainali ya Klabu Bingwa Barani Uropa.

Hata hivyo, Dembele amewaonya wenzake kutoidharau Lyon kwa kuwa ni timu ambayo msimu imeendelea kufanya kweli katika ligi ya nyumbani (Ligue 1) na inajivunia wachezaji nyota kama Fekir, Ferland Mendy na Moussa Dembele.

‘Lyon inawachezaji wazuri ambao hatawaliwaongoza kuinyuka Manchester City na PSG kwenye mashindano na UEFA na Ligue 1. Lazima tulenga kuyafunga magoli yetu iwapo tunatarajia kupata ushindi,” akasema Dembele.