Michezo

Messi kupoteza mkewe asipomkoma Miss BumBum

November 12th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ANTONELLA Roccuzzo ambaye ni mkewe Lionel Messi amemtaka mfumaji huyo wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina kukatiza kabisa mawasiliano yote na kipusa Suzy Cortez au la, aivue pete ya ndoa aliyomvisha rasmi mnamo Juni 2017.

Kulingana na gazeti la The Sun, Antonella anahisi kwamba mumewe huenda akashawishika kutoka kimapenzi na Suzy, mshindi wa zamani wa taji la Miss BumBum, ambaye amekuwa na mazoea ya kuvua nguo na kusalia uchi wa mnyama kila mara Messi anapokivunia kikosi chake ufanisi mkubwa. “Antonella hali halali akiwazia mbinu za kumzuia Messi kuchepuka na Suzy ambaye amekuwa akimwandama sana mitandaoni!”

Mnamo Septemba 2017, Antonella alimshinikiza Messi kutia chale zenye michoro ya midomo yake ( Antonella) pajani ili iwe ishara ya kiwango cha ukomavu wa penzi lao!

Pindi alipochora ‘midomo’ ya mkewe katika sehemu za paja lake la kushoto, ilimjuzu Messi kutuma picha kwenye mtandao wake wa Instagram ili kuiridhisha nafsi ya mkewe ambaye kwa sasa ametishia kumtema iwapo mvamizi huyo ataendelea kumruhusu Suzy kumtia kishawishini.

Kilichomkoroga nyongo zaidi Antonella kiasi cha kumuonesha mumewe kadi ya njano, ni hatua ya Messi kumruhusu Suzy kumfikia tena katika mtandao wake wa Instagram baada ya shinikizo la mashabiki kufanikisha kampeni za #UnBlockMeMessi.

Suzy alianzisha kampeni za kumtaka Messi kumpa upya idhini ya kumfikia kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa Agosti 2018 na akafaulu.

“Messi asante sana kwa kuniruhusu tena kukufikia kwenye Instagram. Hata hivyo, kiu yangu itazima tu iwapo utakitalii kisima,” akaandika mwanamitindo huyo mzawa wa Brazil.

Karibuni, Suzy amekuwa mwepesi wa kupakia tena picha zake za uchi mitandaoni kisha kumtumia Messi kupitia Instagram huku akimshawishi kufanya hima na kuanza kulimenya tunda lake.

“Messi achana na mwendo wa kobe katika hili suala la penzi. Jipu lapuma sana, nakusubiri ulitumbue. Kumbuka niliahidi kukupa ufunguo wa hili buyu la asali, uchovye kiasi chako popote na vyovyote upendavyo,” akaandika Suzy katika miongoni mwa jumbe zilizompasua kifua Antonella.

Hatua ya Suzy kutafuta upya hifadhi ya penzi lake motomoto kwa Messi inajiri miezi kadhaa baada ya kipusa huyo kupuuzwa na Neymar Jr, Philippe Coutinho na Gerard Pique ambaye mkewe mzawa wa Colombia, Shakira, 41, anamzidi kwa miaka 10 kiumri.

Suzy ndiye aliyetawazwa mshindi wa Miss BumBum mnamo 2015. Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka kwa mwanamke mwenye makalio ‘bora’ na makubwa zaidi nchini Brazil.

Kwa pamoja na mkewe, Messi amejaliwa watoto watatu – Thiago, Mateo na Ciro aliyezaliwa mnamo Machi 2018.