Messi kusubiri zaidi kuchezea PSG baada ya kutambulishwa rasmi kwa mashabiki wa kikosi hicho

Messi kusubiri zaidi kuchezea PSG baada ya kutambulishwa rasmi kwa mashabiki wa kikosi hicho

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi atatambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Paris Saint-Germain (PSG) hii leo japo hatachezeshwa na kikosi hicho katika mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) dhidi ya Strasbourg.

Messi, 34, alijiunga na PSG kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kubanduka kambini mwa Barcelona. Kufikia sasa, ameshiriki vipindi viwili pekee vya mazoezi tangu aongoze Argentina kutwaa taji la Copa America mnamo Julai 2021.

Messi atatambulishwa kwa mashabiki pamoja na wanasoka Sergio Ramos, Gianluigi Donnarumma, Georginio Wijnaldum na Achraf Hakimi kabla ya PSG kushuka dimbani kupepetana na Strasbourg ugani Parc des Princes.

“Tutachukua muda kabla ya kuanza kumchezesha hatua kwa hatua. Sasa anajitahidi kufahamiana na wenzake na kuzoea mazingira mapya. Nimezungumza naye na anafurahia maisha hapa. Ataanza kuchezea PSG hivi karibuni,” akasema kocha wa PSG, Mauricio Pochettino.

Messi ambaye ni mshindi mara sita wa taji la Ballon d’Or, hajawahi kuchezea klabu yoyote nyingine mbali na Barcelona.

Chini ya Pochettino ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Tottenham Hotspur, PSG walikamilisha kampeni za Ligue 1 mnamo 2020-21 katika nafasi ya pili nyuma ya Lille. Walianza kampeni zao za muhula huu kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Troyes.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WASONGA: Serikali ikubali wazo la ODM uchumi ufunguliwe

Baba na watoto washtakiwa kwa wizi wa Sh.54Milioni