Michezo

Messi 'kususia' mazoezi kambini mwa Barcelona huku akikaribia kutua Manchester City

August 30th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MACHO yote ya mashabiki yataelekezwa kesho Jumatatu uwanjani Camp Nou, Uhispania kujua iwapo nyota Lionel Messi atakuwa sehemu ya wanasoka wa Barcelona watakaorejea kambini kujifua kwa minajili ya msimu ujao wa 2020-21.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Messi anatarajiwa kususia mpango huo baada ya wakala na baba yake mzazi kuwasiliana na kocha Pep Guardiola kuhusu uwezekano wa Manchester City kumsajili fowadi na nahodha huyo wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina.

Mnamo Agosti 25, Messi, 33, aliwataka Barcelona kumwachilia abanduke ugani Camp Nou ilia sake hifadhi mpya kwingineko muhula huu wa uhamisho.

Nyota huyo aliwatumia vinara wa Barcelona barua ya faksi akieleza kwamba angependa kifungu kwenye kandarasi yake kinachompa idhini ya kuagana na miamba hao wa soka ya Uhispania bila ada yoyote kitekelezwe haraka iwezekanavyo.

Messi ambaye ni mshindi mara sita wa taji la Ballon d’Or ambalo mchezaji bora zaidi duniani hupokezwa, aliwajibishwa na Barcelona kwa mara ya kwanza mnamo 2004 na amewaongoza miamba hao kunyanyua ubingwa wa UEFA mara nne.

Alijiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13 pekee na amefungia waajiri wake jumla ya mabao 634 kutokana na mechi 730 zilizopita na ndiye mwanasoka anayejivunia historia ya mafanikio makubwa zaidi ugani Camp Nou.

Akisalia na mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake na Barcelona, Messi amenyanyulia kikosi hicho jumla ya mataji 33.

Licha ya Messi kutaka kuondoka ugani Camp Nou, Barcelona wamesisitiza kwamba kifungu ambacho Messi anataka kutumia ili aagane nao kilipitwa na wakati na kwa hivyo anasalia kuwa mchezaji wao hadi mwishoni mwa mwaka wa 2021.

Kwa mujibu wa Barcelona, yeyote anayetaka kumsajili Messi kwa sasa atalazimika kuweka mezani kima cha Sh89 bilioni ili kuwashawishi kumwachilia.

Mbali na Man-City na PSG, kikosi kingine kinachohusishwa na Messi ni Juventus ambao wanapania kumtumia nyota Cristiano Ronaldo kumshawishi Messi kutua jijini Turin kucheza pamoja naye kambini mwa miamba hao wa soka ya Italia (Serie A).

Kwa mujibu wa gazeti la Evening Standard, Man-City wapo radhi kuwapa Barcelona beki Jose ‘Angelino’ Esmoris au Eric Garcia ili kumpata Messi. Hii ni baada ya Guardiola kufutilia mbali uwezekano wa kuwapa Barcelona wanasoka Bernardo Silva na Gabriel Jesus wanaoviziwa na Koeman.

Hata hivyo, Bartomeu amesisitiza kwamba hataki kuwa rais wa kwanza wa Barcelona kumshuhudia Messi akibanduka ugani Camp Nou licha ya mwanasoka huyo kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kuungana na Guardiola aliyewahi kumnoa kambini mwa Barcelona kati ya 2008 na 2012.

Koeman kwa upande wake ameshikilia kuwa kuondoka kwa Messi kutawezesha wachezaji Frenkie de Jong, Miralem Pjanic, Ousmane Dembele, Philippe Coutinho, Gerard Pique na Marc-Andre Ter Stegen kukomaa zaidi kitaaluma ugani Camp Nou chini ya uongozi wa fowadi Antonio Griezmann.

“Kwa heshima zote, Griezmann lazima arejee kucheza katika nafasi aliyozoea kambini mwa Barcelona. Uwepo wa Messi na Luis Suarez umemnyima fursa hiyo kwa kipindi kirefu. Hapa ndipo msaada na ushauri wa kocha unahitaji zaidi,” akasema Koeman.