Michezo

Messi, Ronaldo, Neymar ndio wanaspoti matajiri zaidi duniani

June 13th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

NEW YORK, Amerika

NYOTA Lionel Messi wa Barcelona ndiye mwanamichezo anayelipwa pesa nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote mwingine duniani.

Kulingana na utafiti wa jarida la Forbes uliofanyiwa wachezaji 100 matajiri zaidi, nyota huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 31 alipokea Sh19 bilioni katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Fowadi mzawa wa Ureno, Cristiano Ronaldo wa Juventus ya Italia, anashikilia nafasi ya pili baada ya kulipwa Sh16 bilioni huku mshambuliaji chipukizi Neymar Jr wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Brazil akijivunia nafasi ya tatu kwa malipo ya Sh15.8 bilioni.

Mwaka 2018, mchezaji aliyelipwa fedha nyingi zaidi kuliko wote duniani alikuwa bondia Floyd Mayweather, lakini ameshuka katika orodha hiyo ya kimataifa miongoni mwa wanaspoti wanaoshikilia nafasi za juu kutoka mataifa 25 baada ya kupokea malipo ya Sh42.7 bilioni.

Pigano pekee la bondia huyo tangu Agosti 2017 lilikuwa dhidi ya Tenshin Nasukawa wa Japan ambalo lilifanyika Desemba 2018.

Messi ndiye mwanasoka wa pili kuwa juu katika viwango hivyo baada ya Ronlado, na ndiye mwanasoka pekee miongoni mwa wanaspoti tofauti kuchukua namba moja tangu orodha hiyo ianzishwe mwaka 1990.

Ni mara ya kwanza kwa mchezaji wa soka kuwekwa miongoni mwa watu watatu wanaolipwa vizuri zaidi duniani.

Amerika

Kadhalika, Messi ni miongoni mwa wanariadha 38 wasiotoka Amerika kwenye orodha hiyo, huku wanamichezo nyota 62 wa Amerika wakishikilia nafasi za juu katika orodha hiyo.

Shirika la Mchezo wa Vikapu Amerika (NBA) ndilo linaloongoza kwa kuwa na wachezaji wengi zaidi kwenye orodha hiyo, likiwa na wachezaji 35, huku Le Bron James wa LA Lakers akiongoza orodha ya wachezaji wanaolipwa zaidi. Anashikilia nafasi ya nane akilipwa Sh13.3 bilioni, mbele ya Stephen Curry wa Golden Sate Worriors na Kevin Durant.

Kulingana na orodha hiyo iliyochapishwa juma hili, Serena Williams ni mwanamke pekee kati ya watu 100 walioorodheshwa kwa kiasi cha Sh4.5 bilioni. Mshindi wa Dunia mara tano wa mbio za Formula 1 Lewis Hamilton na mshindi wa zamani wa masumbwi uzani wa juu, Anthony Joshua ndio wanaspoti wanaolipwa vizuri zaidi nchini Uingereza, wakichukuwa katika nafasi ya 13 kutokana na malipo yao ya Sh8.2 bilioni.

Jarida hilo la biashara hujumuisha malipo ya wanariadha kwa kujumlisha fedha za malipo ya tuzo, mshahara na nembo walizoidhinisha kati ya Juni 2018 na Juni 2019. Kiungo Paul Pogba wa Manchester United ndiye mwanasoka anayelipwa zaidi katika EPL.