Messi sasa mali rasmi ya PSG baada ya kutia saini mkataba wa miaka miwili

Messi sasa mali rasmi ya PSG baada ya kutia saini mkataba wa miaka miwili

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi amesajiliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuagana na Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 pia ana fursa ya kurefusha kandarasi hiyo kwa mwaka mmoja zaidi iwapo atahiari kuendelea kuchezea PSG baada ya mkataba wa sasa kutamatika mwishoni mwa 2023.

Messi aliondoka Barcelona – klabu ya pekee ambayo amechezea katika taaluma yake ya usogora – kwa sababu kikosi hicho hakikuwa na uwezo wa kumdumisha kimshahara kulingana na kanuni za La Liga kuhusu matumizi ya fedha miongoni mwa klabu (financial fair play rules).

“Nina hamu ya kuanza maisha mapya kitaaluma jijini Paris. Malengo ya kikosi hiki yanawiana pakubwa na maazimio yangu binafsi,” akasema sogora huyo raia wa Argentina.

“Nafahamu utajiri wa vipaji vya soka kambini mwa PSG. Nitapania pia kushirikiana na kila mmoja wao ili kuvunia klabu hii kitu spesheli kitakachokuwa zawadi ya kuridhisha mashabiki uwanjani Parc des Princes,” akasema Messi.

Kwa upande wake, rais Nasser al-Khelaifi wa PSG alisema: “Ni tija na fahari tele kwamba Messi ameteua kujiunga na PSG. Tuna furaha kubwa kumkaribisha pamoja na familia yake jijini Paris.”

Akichukuliwa kuwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi duniani, Messi alifungia Barcelona jumla ya mabao 672 kutokana na mechi 778 tangu ajiunge na kikosi hicho akiwa kinda wa umri wa miaka 13 pekee.

Akiwa fowadi wa Barcelona, Messi alitia kapuni mataji sita ya Ballon d’Or, tuzo ambayo hutolewa kila mwaka kwa mwanasoka bora zaidi duniani. Sogora huyo anajivunia pia kunyanyulia Barcelona jumla ya makombe 35.

Anakuwa mwanasoka wa tano kusajiliwa na PSG muhula huu baada ya kiungo Georginio Wijnaldum, beki Sergio Ramos, kipa Gianluigi Donnarumma na difenda Achraf Hakimi aliyetokea Inter Milan ya Italia.

Messi ambaye atavalia jezi nambari 30 kambini mwa PSG, atashirikiana na Neymar Jr pamoja na Kylian Mbappe kwenye safu ya mbele ya PSG. Mbappe na Neymar ndio wanasoka ghali zaidi wa muda wote duniani.

Messi huenda akawajibishwa na PSG ya kocha Mauricio Pochettino kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 14, 2021 wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) dhidi ya Strasbourg uwanjani Parc des Princes.

Mbali na PSG, vikosi vingine vilivyokuwa vikihusishwa na Messi tangu kitumbua chake kiingie mchanga kambini mwa Barcelona ni Manchester City na Chelsea.

Kuwapo kwa Messi, Neymar, Mbappe, Mauro Icardi na Angel di Maria kambini mwa PSG kunafanya klabu hiyo kuwa kikosi kinachojivunia mafowadi matata zaidi duniani.

Kwa kutua PSG, Messi anaungana na wanasoka Leandro Paredes na Di Maria walioshirikiana naye mnamo Julai 2021 kuzolea Argentina taji la kwanza la Copa Amerika baada ya miaka 28.

PSG sasa wana kila sababu ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ikizingatiwa kwamba mabingwa hao mara tisa wa Ligue 1 ndicho kikosi kinachojivunia wavamizi bora zaidi duniani.

Japo azma ya kutawala soka ya UEFA ndiyo ilikuwa sababu kuu ya kusajiliwa kwa Neymar, PSG wamekuwa wakibanduliwa mapema kwenye kampeni za kipute hicho.

Baada ya kulemewa na Bayern Munich kwa kichapo cha 1-0 kwenye fainali ya UEFA mnamo 2019-20, PSG ilidenguliwa na Manchester City msimu uliopita kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye nusu-fainali ya kipute hicho ambacho hawajawahi kukishinda.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Afueni ya muda kwa Zuma, korti ikiahirisha kesi

AFYA: Vidonda vya tumbo