Michezo

Metro Sports yaamka Super 8

May 7th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

BAADA ya Metro Sports kuteleza mara tano hatimaye ilifanikiwa kuandikisha ushindi wa tatu iliposhinda 1-0 mbele ya Githurai Allstars kwenye mechi ya kipute cha Premier Eight Premier League (S8PL) iliyochezewa Stima Club, Nairobi.

Ufanisi wa Metro Sports uliisaidia kufuta mkosi wa kuambulia patupu ndani ya mechi tano mfululizo.

Matokeo hayo ni pigo kwa Githurai Allstars inayokamata nafasi ya pili kwa kuzoa alama 14 sawa na Shaurimoyo Sportiff tofauti ikiwa idadi ya mabao baada ya kila moja kupiga mechi tisa.

Kocha wa Githurai Allstars, Fredrick Ochieng aliponda waamuzi waliosimamia patashika hiyo na kudai walipendelea upande mmoja.

”Kusema kweli waamuzi wameibuka mwiba kwetu maana wamechangia vijana kufanya vibaya kupoteza patashika moja na kutoka nguvu sawa mchezo mmoja,” alisema. Licha ya kipigo hicho kocha huyo alisema bado wanapania kujikakamua kwenye juhudi za kupigania ubingwa wa ngarambe ya msimu huu.

Mchezaji wa Metro Sports (kulia) akijaribu chenga mwenzake wa Githurai Sports kwenye mechi ya S8PL iliyopigiwa Stima Club, Nairobi. Metro ilishinda bao 1-0. Picha/ John Kimwere

Metro Sports ilizoa ushindi huo kupitia bao lililotingwa na Michael Ochieng. Naibu kocha wa Metro Sports, David Mbugua alisema “Haikuwa mteremko kwetu kuzima wenyeji wetu ila nashukuru vijana kwa kazi nzuri waliofanya baada ya kujituma kiume dimbani.”

Kwenye mfululizo wa mechi hizo, Declerck Shivachi ilifanikiwa kupiga moja safi na kubeba Dagoretti Former Players kudunga NYSA bao 1-0. Nao wasomi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) walikanyanga Meltah Kabiria kwa mabao 4-2, nayo Lebabon FC ililamishwa sakafu ilipokubali kulala kwa bao 1-0 mbele ya MASA. Nao wanasoka wa Mathare Flames walitoka nguvu sawa bao 1-1 na Shaurimoyo Sportiff.

Kwenye msimamo wa kipute hicho mabingwa watetezi, Jericho Allstars ingali kifua mbele kwa kufikisha alama 22 kutokana na mechi tisa.