Michezo

Mezeni wembe, De Gea awafokea wakosoaji

September 25th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MNYAKAJI wa Manchester United David De Gea amewashtumu wakosoaji na maadui wake akiwataka wameze maneno yao baada ya kushinda tuzo ya kipa bora ulimwenguni wakati wa kutolewa kwa tuzo za FIFA Best Awards jijini London usiku wa Septemba 24.

“Ni kawaida kwangu kutowasikiza watu wanaonisabasi au kuzungumza  mabaya kunihusu. Ninamakinikia taaluma yangu ili kuwezesha timu yangu kufanya vizuri wakati wao umbeya umewajaa midomoni. Huwa sina muda wa kusikiza mambo mengi ya upuzi wanayoyasema,” akasema nyani huyo mahiri.

De Gea ambaye  zamani alisakatia Atletico Madrid ya Uhispania alimpiku kipa wa zamani wa Chelsea ambaye sasa anadakia Real Madrid Thabbaut Cortouis kutwaa tuzo hiyo ya hadhi.

Aidha Mhispania huyo alitajwa langoni katika kikosi kilichojaa mastaa kilichounga na kukamilisha orodha ya wanadimba 11 bora walioteuliwa na Shirikisho la soka duniani FIFA wakati wa hafla hiyo.

Wachezaji wengine katika kikosi hicho walikuwa Dani Alves, Sergio Ramos, Raphael Varane, Marcelo, N’Golo Kante, Luka Modric, Eden Hazard, Kylian Mbappe, Leo Messi na Cristiano Ronaldo.

Wakati uo huo mkufunzi mkongwe Fabio Capello amewakemea vikali mshambulizi wa Juventus Cristiano Ronaldo na mwenzake wa Barcelona Leonel Messi kwa kukosa kuhudhuria sherehe hizo zilizomshuhudia kiungo wa Real Madrid raia wa Croatia Luka Modric akitawazwa mchezaji bora duniani.

“Kukosa kwa Ronaldo na Messi ni ukosefu mkubwa wa heshima kwa wachezaji wenzao, shirikisho la soka na fani nzima ya soka. Hata kama wamekuwa wakishinda tuzo hiyo na mara hii wakabwaga wangehudhuria tu. Katika maisha kuna kushinda na kupoteza na unatakiwa kuwa mstarabu unaposhindwa,” akasema Mwitaliano huyo aliyewahia kunoa Juventus, Real Madrid na timu ya taifa ya Uingereza, The Three Lions.