Mfahamu Jarred Gillett ambaye sasa atakuwa refa wa kwanza wa kigeni kupuliza kipenga katika mechi za EPL

Mfahamu Jarred Gillett ambaye sasa atakuwa refa wa kwanza wa kigeni kupuliza kipenga katika mechi za EPL

Na MASHIRIKA

JARRED Gillett atakuwa refa wa kwanza asiyekuwa raia wa Uingereza kupuliza kipenga katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kibarua chake cha kwanza ni mechi itakayowakutanisha Watford na Newcastle United ligini mnamo Septemba 25, 2021.

Gillett, 34, alipandishwa ngazi hadi kiwango cha Select Group 1 na Shirikisho la Marefa la Soka ya Kitaaluma (PGMOL) kabla ya kampeni za msimu huu wa 2021-22 kuanza.

Hadi alipoaminiwa fursa ya kuwa mwamuzi wa mechi za EPL, alikuwa akishughulikia na masuala ya tekonolojia ya VAR na kwa wakati fulani akapata fursa ya kupuliza kipenga katika mechi mbili za Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Gillett alianza kufanya kazi ya urefa nchini Uingereza mnamo 2019 baada ya kuagana na Ligi Kuu ya Australia (A-League).

Kwa mujibu wa vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Gillett atakuwa refa wa kwanza wa kigeni kuwahi kusimamia michuano ya Ligi Kuu.

Ingawa refa wa zamani wa EPL, Dermot Gallagher, alizaliwa Ireland na kuhamia Uingereza akiwa na umri wa miaka 16, alichukuliwa kuwa miongoni mwa wawakilishi wa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) na akaruhusiwa kusimamia mechi kati ya Ireland na Urusi mnamo 2002.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Keter, Munyes wakasirisha maseneta kwa kudinda kufika mbele...

Dereva amrejeshea mwanafunzi laputopu na Sh20,000...