Kimataifa

Mfalme Charles aahirisha shughuli rasmi baada ya kugunduliwa anaugua saratani

February 5th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MFALME Charles III wa Uingereza amethibitishwa kuugua saratani,  yalisema makao ya kifalme ya Buckingham, kwenye taarifa Jumatatu.

Makao hayo hayakueleza aina ya saratani ambayo kiongozi huyo alithibitishwa kuugua, ijapokuwa ilikanusha kwamba alipatikana akiugua saratani ya kibovu.

Yalieleza kuwa saratani hiyo iligunduliwa kwenye “ukaguzi wa kawaida wa kimatibabu na madaktari wake”.

Yalieleza kuwa “Mfalme ana matumaini makubwa kuhusu matibabu yake na anatarajia kurejelea kazi zake kama kawaida hivi karibuni”.

“Mfalme ataahirisha hafla zake za umma. Inatarajiwa kuwa maafisa wa ngazi za juu wa kifalme watamwakilisha kwenye hafla hizo anapoendelea kupata matibabu,” ikaeleza taarifa hiyo.

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu kiwango chake au aina ya matibabu atakayopata.

Mfalme Charles, 75, alirejea jijini London kutoka eneo la Sandringham Norfolk, Jumatatu asubuhi, na makao ya kifalme yalisema ameanza matibabu yake kama mgonjwa wa kawaida.

Ijapokuwa kiongozi huyo atasitisha hafla za umma, ataendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kama kiongozi wa nchi, yakiwemo utiaji saini wa stakabadhi muhimu zinazohusu masuala ya nchi na kuhudhuria mikutano muhimu ya faragha.

Kiongozi huyo alihudhuria ibada ya kanisa katika eneo la Sandringham, mnamo Jumapili, na hata kuusalimia umati wa watu uliokuwa umefika kwa mbali.

Wiki moja iliyopita, kiongozi huyo alifanyiwa ukaguzi wa kimatibabu wa saratani ya kibovu katika hospitali moja jijini London.

Kiongozi huyo alizuru nchini Kenya mwezi Oktoba mwaka uliopita.