HabariSiasa

Mfalme wa Kisii

January 13th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na RUTH MBULA

WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i, ameibuka kuwa mfalme mpya wa jamii ya Wakisii, kiasi cha wabunge wa eneo hilo kuanza kumtii huku akifuata nyayo za vigogo wa kisiasa waliokuwa na usemi mkubwa katika jamii hiyo.

Macho yote ya sasa yanaelekezwa kwa waziri huyo uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022 ukikaribia, dalili zikionyesha kuwa wanasiasa wakuu akiwemo kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga wanamchangamkia.

Bw Matiang’i kwa sasa anaonekana kuwa mrithi wa waziri wa zamani, Bw Simon Nyachae ambaye alikuwa kigogo wa kisiasa na msemaji wa jamii hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja, baada ya kifo cha aliyekuwa mshikilizi wa wadhifa huo Lawrence Sagini.

Ndiposa mnamo Aprili mwaka jana, Baraza la Wazee wa Jamii ya Abagusii lilimtawaza Dkt Matiang’i kuwa msemaji wa jamii hiyo katika nyanja za kisiasa, kijamii na kimaendeleo na kuibua uvumi kuwa atawania urais 2022.

Hii ndiyo maana kufikia sasa, sita kati ya wabunge tisa kutoka eneo pana la Gusii ambao wamekuwa wakipigia debe azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao, wamegura kambi hiyo na kujiunga na ile ya Dkt Matiang’i.

Katika siku za hivi karibuni, wandani hao wa Dkt Ruto wamekuwa wakihudhuria mikutano ya Dkt Matiang’i, mfano mzuri ukiwa mkutano wa kuvumisha ripoti ya maridhiano (BBI) mjini Kisii mnamo Ijumaa.

Wabunge wa hivi punde kujinga na kambi ya Dkt Matiang’i ni Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba) na Oroo Oyioka (Bonchari) ambao walitangaza kujitenga na Dkt Ruto walipojiunga na zaidi ya wajumbe 3,000 waliohudhuria mkutano huo.

Wandani wengine wa naibu huyo wa rais waliofika mkutanoni hapo kuungana na Matiang’i ili wasipoteze viti vyao 2022 ni Richard Tong’i (Nyaribari Chache) na Profesa Zadoc Ogutu (Bomachoge Borabu).

Mbunge wa Kuria Mashariki Marwa Kiyatama ambaye ni mshiriki mkuu wa Dkt Ruto katika Kaunti ya Migori pia aliibua minong’ono kutoka kwa wakazi kwa kuhudhuria mkutano huo.

Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, ambaye amekuwa akiongoza jumbe kadhaa kutoka Kisii kwenda kumtembelea Dkt Ruto katika makazi yake ya Karen, Nairobi na nyumbani kwake Sugoi, pia ameonekana kulegeza msimamo wake na kudai kuwa hakuna uhasama wowote kati yake na Dkt Matiang’i na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Nyota ya Dkt Matiang’i ilianza kung’aa mapema mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta alipomkweza cheo na kuwa Mkuu wa Mawaziri wote. Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri na Kusimamia na Kushirikisha utekelezaji wa miradi ya serikali kuu kitaifa hadi ngazi za mashinani.

Wadhifa huo vilevile umemfanya kuwa kivutio kwa wanasiasa kutoka eneo la Gusii ambao sasa wanamsukuma kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022, japo hajatangaza kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Na mnamo Mei, 2019, Bw Odinga alidokeza kuwa huenda akamwidhinisha Dkt Matiang’i kwa wadhifa wa urais “wakati ukifikia”.

Huku akimtaja waziri huyo kama mwana wake ambaye alimjua tangu zamani, Bw Odinga alisema kumtawaza wakati huu kutaharibu malengo ya muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, almaarufu handisheki.

“Huyu ni kijana mchapakazi. Kwa hivyo, msinikumbushe kile ambacho ninapaswa kufanya. Lakini wakati haujatimu. Tulieni,” Bw Odinga akawaambia waombolezaji kwenye mazishi ya aliyekuwa waziri msaidizi Hezron Manduku.

Ni wakati huo ambapo mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Bw Richard Onyonka aligura kambi ya Naibu Rais na kutangaza kwamba anaunga mkono Dkt Matiang’i na handisheki.

Wabunge kutoka eneo la Gusii ambao sasa wamesalia katika kambi ya Dkt Ruto ni Joash Nyamoko (North Mugirango), Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Vincent Kemosi (West Mugirango), Silvanus Osoro (South Mugirango) na Alpha Miruka (Bomachoge Chache). Naye Mbunge wa Bobasi Innocent Obiri anaonekana kuwa na msimamo vuguvugu maadamu haijulikani anaegemea mrengo upi.