Kimataifa

Mfalme wa Swaziland abadili jina la taifa hilo hadi eSwatini

April 22nd, 2018 1 min read

MBABANE, SWAZILAND

Mfalme Mswati wa Swaziland amebadilisha jina la taifa kuwa eSwatini.

“Ninataka kutangaza kuwa Swaziland itarudia jina lake la awali Eswatini,” alitangaza Alhamisi wakati wa sherehe za kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, na miaka 50 baada ya taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.

“Mataifa ya Afrika baada ya kupata uhuru yalirejea kutumia majina yao ya awali kabla ya ukoloni. Hivyo kuanzia leo taifa hili litaanza kuitwa Ufalme wa eSwatini,” aliongeza.

Taifa hilo ndogo sana kusini mwa Afrika lilipata uhuru 1968 baada ya kutawaliwa na Uingereza. Lakini halikubadilisha jina lake kama mataifa mengine yalivyofanya.

Jina hilo linamaanisha “eneo la Swazi”, hivyo, eSwatini ni jina la taifa hilo kwa lugha ya Swazi.

Jina Swaziland liliwaudhi baadhi ya raia kwa sababu lilitokana na mchanganyiko wa lugha za Swazi na Kiingereza.

Hatua hiyo ilikuwa imejadiliwa kwa miaka kadhaa. Mwaka wa 2015, wabunge walitathmini suala hilo kwa kina.

Mfalme Mswati alitumia jina hilo mpya katika hotuba rasmi za awali.

Mfalme huyo aliyepewa mamlaka 1986 akiwa na miaka 18 kuambatana na tamaduni na ni taifa la kipekee Afrika kuongozwa na mfalme.

Tangu 1973, Swaziland imepiga marufuku vyama vya kisiasa kushiriki uchaguzi, ingawa vingalipo.

Ili kuwania wadhifa wa kisiasa, wawaniaji huwa wanatumia tiketi ya kibinafsi halafu wanaidhinishwa na mfalme kama wabunge.

Taifa hilo ambalo lina watu 1.3 milioni lina asilimia kubwa zaidi ulimwenguni ya virusi vya Ukimwi, ambapo asilimia 27 ya watu wazima wameambukizwa.

Kubadilishwa kwa jina kunamaanisha kuwa katiba ya nchi hiyo pia itaandikwa tena na huenda mabadiliko ya majina yakashuhudiwa katika idara ya polisi ya inayofahamika kam Royal Swaziland Police, jeshi la Swaziland na Chuo Kikuu cha Swaziland.