Habari

Mfano mbaya!

September 11th, 2020 3 min read

BENSON MATHEKA Na RUTH MBULA

VIONGOZI wakuu nchini Alhamisi waliendelea kuwa mfano mbaya kwa kuvunja sheria na kupuuza kanuni za kuzuia kuenea kwa maambukizi ya Covid-19.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga walihutubia mikutano maeneo mbalimbali iliyokuwa na misongamano, kusalimia watu kwa mikono na kuwapiga pambaja.

Vigogo hao walionyesha mapuuza makubwa ambayo yaliwaacha Wakenya wakiulizana iwapo corona imekwisha nchini au kanuni hizo zinapaswa kuzingatiwa na wananchi wa kawaida pekee.

Kinaya ni kuwa kwenye mkutano jana, Baraza la Mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais Kenyatta lilitoa mwito kwa Wakenya kuendelea kuzingatia kanuni za MoH ambazo ni pamoja na kuepuka misongamano, kuvaa barakoa na kunawa mikono

Mnamo Jumanne, Waziri Msaidizi wa Wizara ya Afya (MoH), Rashid Aman, alionya kwamba ingawa visa vya maambukizi vimepungua, Kenya haijaangamiza virusi hivyo.

“Ingawa tumeshuhudia idadi ya visa ikipungua Nairobi na Mombasa, maambukizi yameendelea katika kaunti za mashambani na kwa hivyo hatufai kulegeza kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi hivi,” alisema Bw Aman.

Mnamo Jumatano, Rais Kenyatta, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhimiza wananchi kuheshimu maagizo yake ya kukabiliana na virusi vya corona, alijipuuza mwenyewe kwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika eneo la Ruaka, Kaunti ya Kiambu. Kwenye mkutano huo wananchi hawakuzingatia kanuni za kujikinga na corona kwani walisongamana na wengi wao hawakuwa na barakoa.

Hii ni licha ya kuwa anapofanya mikutano rasmi na marais wenzake ama mingine ya kimataifa na kiserikali amekuwa akitumia video katika juhudi za kuzuia maambukizi yanayotokana na watu kutagusana.

Naibu Rais William Ruto naye aliendeleza upuuzaji wa tahadhari za corona kwa kumuiga bosi wake alipohutubia halaiki kubwa mjini Kisii jana.

Mnamo Jumapili iliyopita, Dkt Ruto alikuwa mjini Athi River ambako pia alionyesha kutojali maisha ya wakazi alipowahutubia wakiwa wamesongamana.

Wiki iliyopita Dkt Ruto pia alitembelea kaunti za Taita Taveta na Mombasa ambako aliwahutubia wakazi ambao hawakuzingatia kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona.

Hii ni kinyume na awali ambapo amekuwa akijidai kuzingatia kanuni za serikali anapoandaa mikutano nyumbani kwake hasa ya wajumbe wa kidini na kisiasa, ambako ofisi yake husisitiza wanazingatia kanuni za MoH.

Bw Odinga naye hakuachwa nyuma katika mashindano ya wakuu kuvunja tahadhari za Covid-19, kwani akiwa Taita Taveta aliwahutubia wananchi ambao hawakutilia maanani kanuni za kujikinga.

Bw Odinga pia aliwasalimia watu kwa mkono na kuwapiga pambaja. Hii ni licha ya MoH kuendelea kushauri Wakenya wakome kusalimiana kwa mikono, kupigana pambaja na kukaribiana.

Wiki jana, mawaziri Keriako Tobiko (Mazingira), Mutahi Kagwe (Afya) na Fred Matiang’i (Usalama) walihudhuria na kuhutubia mkutano Kaunti ya Kajiado.

Tabia hii ya wanaotarajiwa kuwa mstari wa mbele kuheshimu sheria na kuwa mfano mwema wa kuigwa na wananchi inawafanya raia nao kuvunja sheria.

Wahudumu wa matatu waliozungumza na Taifa Leo jana walilalamika kuwa wanalazimishwa kubeba abiria wachache na hali Rais, Naibu Rais, Bw Odinga na mawaziri wanashiriki shughuli zenye misongamano ya watu.

“Huu ni unyanyasaji. Tumeambiwa kubeba abiria wachache huku wao wakiacha watu kusongamana. Hawajali mwananchi,” akasema Eliud Mogaka, dereva wa matatu Nairobi.

Wengine waliohojiwa na Taifa Leo walieleza hisia kali baadhi wakitaja Covid-19 kama janga lililobuniwa na viongozi wakiwa na nia fiche.

“Serikali ilikuwa ikitafuta tu fursa ya kukopa pesa ambazo ni sisi raia ambao tutalipa. Mbona majirani wetu Tanzania hawakuchukua hatua kama Kenya na bado wako salama?” akasema Alex Wafula, mkazi wa Nairobi.

“Walituwekea lockdown ili waweze kuiba pesa polepole tukiwa nyumbani. Polisi nao walipata nafasi ya kutupiga na kuchukua hongo juu ya kafyu na maski,” Joel Mburu, mkazi wa Kiambu akaeleza.

Wengine walieleza hasira wakisema serikali ilieneza hofu miongoni mwa wananchi na kusababisha maelfu kupoteza kazi zao na makampuni kuporomoka.

“Hata mazishi tunakatazwa kwenda na kuwekewa sheria kuwa mtu akifa azikwe hivi ama vile. Wameonyesha wanatuchukulia kama takataka. Nimekasirika sana na viongozi,” akasema Zainab Hussein mtaani Huruma, Nairobi.