HabariSiasa

Mfano wa kuigwa

April 11th, 2020 3 min read

AHMED MOHAMED na VALENTINE OBARA

MAGAVANA watatu wameibuka kuwa mfano wa kuigwa kwa juhudi zao za kukabiliana na virusi vya corona, wakati ambapo wenzao wanalalamikia ukosefu wa fedha kuandaa kaunti zao kukabili janga hilo endapo hali itakuwa mbaya zaidi.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho, mwenzake wa Kitui Charity Ngilu na Prof Kivutha Kibwana wa Makueni wameonyesha kuwa kila kiongozi anaweza kuchukua hatua za kuwafaa wananchi.

Huku hayo yakijiri, kuna magavana ambao wamedai hawana uwezo hata wa kusambaza maski kwa wahudumu wa boda boda, wakilalamika kuwa serikali kuu imechelewa kuwatumia fedha!

Katika Kaunti ya Nyeri, Gavana Mutahi Kahiga amelaumiwa vikali kwa kutumia maelfu ya pesa kuweka picha zake kwenye chupa za sanitaiza aliyopewa kama msaada na kiwanda cha Kibos Sugar Company.

Gavana Wycliffe Wangamati wa Bungoma naye yumo motoni kwa madai kuwa serikali yake ilinunua mitungi 600 ya lita 20 ya maji ya kunawa mikono, kila moja kwa Sh10,000. Mitungi hiyo kwa kawaida huuzwa kati ya Sh50 na Sh100.

Lakini Bw Joho, Bi Ngilu na Prof Kibwana wametoa matumaini kwa Wakenya kuwa bado kuna viongozi wanaoweza kutegemewa.

Serikali kupitia kwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe tayari imemtambua Bw Joho kwa juhudi zake kabambe na akazitaka serikali zote za kaunti kuiga Bw Joho.

“Nataka kuishukuru serikali ya Mombasa na hususan gavana wao kwa juhudi zake. Ni ombi langu kwa serikali zile nyingine zijitolee kuweka juhudi kama hizo ili kusaidia watu wetu,” akasema Bw Kagwe.

Bidii ya watatu hao imefikia kiwango cha wakazi wa kaunti nyingine, ambazo magavana wake wamelaza damu na kazi yao ni kulalamikia ukosefu wa fedha.

Ndani ya muda wa wiki mbili tangu kuongezeka kwa visa vya kusambaa kwa virusi vya corona, Bw Joho ameweka mikakati tofauti ya kuhakikisha kuwa wakazi wake wamelindwa wakati huu mgumu.

“Huu ndio wakati ambapo ni lazima tuweke maamuzi makubwa kwa ajili ya watu wetu ili tuweze kukinusuru kizazi chetu. Ni lazima kama viongozi tuje pamoja kupambana na janga hili,” asema Bw Joho.

Jana, Bw Joho alitangaza kuwa serikali yake imewekeza Sh64 milioni kwa ajili ya upanuzi wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Pwani (CPGH) kwa kuongeza vitanda 150 vya wagonjwa wa corona, mbali na vile 19 vya awali pamoja na dawa.

Bw Joho ameonyesha ustaarabu na ukomavu kwa kuwashawishi maadui wake kisiasa kuunga mkono juhudi zake za kuwasaidia wakazi wa Mombasa.

Kwa ushirikiano na aliyekuwa mpinzani wake katika kiti cha ugavana Suleiman Shahbal, wamenunua mashine ya kunyunyuzia wakazi wa Likoni dawa za kuua viini wanaopoingia feri.

Mradi wa mashine hizo ambazo zimeekwa pande zote mbili za Kivuko cha Likoni pia umewekwa katika katika Soko la Kongowea.

Sifa nyingine ambayo Gavana Joho amedhihirisha wakati huu wa janga ni uwezo wake kutafuta ufadhili. Hii imemsaidia kupokea mashine 10 za kusaidia wagonjwa kupumua katika CPGH. Alipokea mashine hizo kutoka kwa wafadhili wa Uarabuni ambao ni marafiki zake wa karibu alipowaomba msaada.

Katika kuwatumikia wananchi kwa kujali maslahi yao ya kimsingi, serikali ya Mombasa imetenga Sh200 milioni ambazo zitatumika kuwapa chakula wakazi elfu 200 ambao maskini.

Kwa juhudi zake za kuomba misaada, Gavana Joho tayari amepata vyakula na misaada mingine ya thamani ya Sh100 milioni kutoka kwa matajiri wa kaunti yake za kusaidia juhudi wananchi walio na mahitaji.

“Maafisa wa kaunti wataanza kusambaza chakulka ili kuhakikisha kuwa hakuna mkazi anayekufa njaa wakati huu mgumu. Tutajitolea vyakutosha ili kunusuru watu wetu na Mungu atatusaidia,” akasema Bw Joho.

Huku mradi huo ukianza, Bw Joho alirudi tena katika Kivuko cha Likoni ambapo aliagiza watumizi wote wa kivuko hicho wapewe maski bila malipo.

Katika Kaunti ya Kitui, Bi Ngilu amekuwa mfano kwa kugeuza kiwanda cha utengenezaji nguo cha Kitui kuwa cha kutengeneza maski.

Kiwanda hicho ambacho awali kilikuwa kimepewa zabuni ya kutengeneza sare za maafisa wa serikali kuu kitaifa, kinanuia kutengeneza maski 30,000 kwa siku.

Hatua hiyo imepokea sifa kimataifa hata kutoka kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwani Kenya sasa haitategemea tena uagizaji maski kutoka nchi za nje wakati huu ambapo kuna uhaba kimataifa.

Katika Kaunti ya Makueni, Prof Kibwana, ambaye pia amekuwa akiweka mikakati mbalimbali, amesifiwa kwa kufungua kitengo maalumu cha kuhudumia wagonjwa wa corona.