Habari MsetoSiasa

Mfanyabiashara adai Biwott alikufa na deni lake la Sh6.7 bilioni

March 6th, 2019 1 min read

TITUS OMINDE na CEDRICK KHAYEKA

MFANYABIASHARA mmoja mjini Eldoret, amewasilisha kesi akitaka korti izuie familia ya aliyekuwa waziri wakati wa utawala wa KANU, Bw Nicholas Kipyator Biwott, kugawanya mali yake.

Mfanyabiashara huyo anataka Mahakama Kuu ya Eldoret izuie familia hiyo kugawanya au kuuza mali ya marehemu hadi kesi aliyowasilisha akitaka familia hiyo kumlipa deni la Sh6 bilioni, anazodai kumkopesha marehemu, itaamuliwa.

Bw Barnabas arap Kiprono, al maarufu Lodwar, kupitia kwa wakili wake, J K Chesoo anataka mahakama kuwazuia wasimimizi wa mali ya marehemu ambao ni Destrerio Andati Oyatsi, Kenneth Hamish Wooler Keith na Elizabeth Klem , kuuza wala kugawanya mali hiyo kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi ambapo anadai marehemu pesa hizo zilizoongezeka kwa sababu ya riba ya mkopo.

Bw Kiprono alidai kuwa alimkopesha marehemu Sh382 milioni, na kulingana na mkataba wao, pesa hizo zimezaa riba na kufikia zaidi ya Sh6.7 bilioni.

Aliambia mahakama kuwa alimpa marehemu mkopo wa kwanza wa Sh50 milioni kwa riba asilimia 25 , Novemba 5, 2015. Novemba 11, 2015 alimwongezea Sh35 milioni kwa riba ya asilimia 30.

Pia alimpa Sh10 milioni Januari 9, 2016 na Sh2 millioni Februari 20, 2016.

Vile vile aliambia mahakama alimkopesha Bw Biwott Sh280 milioni kwa riba ya asilimia 18 mnamo Machi 29, 2016 kabla ya kumuongeza Sh5 milioni kwa riba ya asilimia 30 Septemba 2, 2016.