Habari za Kitaifa

Mfanyabiashara aduwaza Bunge kukiri hakujua kilichokuwa kwa magunia aliyouza kama mbolea

April 10th, 2024 2 min read

COLLINS OMULO NA WANDERI KAMAU

MMILIKI wa kampuni iliyopigwa marufuku kwa kusambaza mbolea ghushi nchini, jana aliwashangaza wabunge alipokiri kwamba hana ufahamu kuhusu aina ya mbolea ambayo amekuwa akiiuzia serikali.

Bw Josiah Kariuki, ambaye ndiye mkurugenzi mkuu wa kampuni ya SBL Innovate Manufacturers Limited, aliiambia Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Kilimo kwamba alienda kwa Halmashauri ya Kitaifa ya Kununua Nafaka (NCPB) mnamo Machi 20, 2022 kwa nafasi ya kibiashara ya kusambaza mbolea.

Hili ni baada ya kutumia mbolea kutoka kampuni ya African Diatomite Industries Limited (ADIL), iliyofanya vizuri katika shamba lake lililo katika eneo la Rumuruti, Kaunti ya Laikipia.

Licha ya utata ambao ungetokea baadaye, Bw Kariuki alipewa zabuni hiyo na NCPB.

Aliiambia kamati hiyo, inayoongozwa na mbunge John Mutunga (Tigania Magharibi) kwamba, kwa ushirikiano na ADIL na kampuni yake nyingine—51 Capital Kenya—waliingia kwenye makubaliano ya zabuni na NCPB mnamo Machi 31, 2022 kusambaza bidhaa aina tatu.

Capital 51 Kenya ilisajiliwa rasmi mnamo Februari 6, 2020.

Bidhaa walizokubalina kusambaza ni vifaa vya kuwapa mifugo aina ya 51 capital animal supplements, GPC-Guard na diatomaceous kwa viwango vya magunia ya kilo 25 katika bei ya Sh1,800, Sh1,950 na Sh1,500 mtawalia.

Bidhaa hizo tatu zilikuwa ziuzwe na NCPB kwa bei ya Sh1,980, Sh2,145 na Sh1,700 mtawalia.

Kandarasi hiyo ilikuwa idumu kwa muda wa miaka miwili huku bidhaa hizo zikitathminiwa baada ya kila miezi sita. Hilo ndilo lingeamua kuhusu ikiwa zabuni hiyo ingeendelea au la.

“Tulianza usambazaji wa bidhaa hizo karibu Mei au Juni 2022, ambapo ADIL ilikuwa itengeneze na kusambaza mbolea. Kampuni yangu ilikuwa iiuzie NCPB,” akasema Bw Kariuki, aliyekuwa ameandamana na mawakili saba, wakiwemo Bw Cliff Ombeta na Bw Danstan Omari.

Hata hivyo, Bw Mutunga alimwambia Bw Kariuki kuieleza Bunge jinsi kampuni yake ya ADIL iliingia kwenye mkataba na NCPB bila makubaliano yoyote ya kisheria.

“Nimekuwa nikiuza kile nilimbiwa na Mamlaka ya Kukadiria Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS). Sina uwezo wa kujua bidhaa ninayouza,” akasema, kauli iliyowaacha wabunge katika hali ya mshangao.