Habari Mseto

Mfanyabiashara aitaka bunge limtimue Matiang'i kazini

April 5th, 2018 1 min read

 Na CHARLES WASONGA

MFANYABIASHARA mmoja amelitaka Bunge la Kitaifa kubaini ikiwa Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i anastahili kushikilia afisi ya umma na lipendekeze aondolewe kutoka wadhifa huo.

Bw Mohamud Mohamed Sheik Jumanne aliwasilisha ombi bungeni kutaka wabunge wabaini kuwa Waziri huyo amakiuka katiba na sheria kuhusu maadili na uongozi bora kuhusiana na jinsi alivyoshughulikia sakata ya Miguna Miguna.

“Kwa misingi hiyo, naliomba bunge hili kuanzisha mchakato wa kumwondoa afisini Waziri wa Usalama wa Ndani,” akasema kwenye ombi hilo.

Bw Sheikh alisema Dkt Matiang’i alifeli kuzingatia kiapo chake cha afisi cha kutetea katiba kwa kukaidi amri ya mahakama hali iliyopelekea Jaji wa Mahakama Kuu kumpata na hatia na kumtoza faini ya Sh200,000.

Hii ni baada ya Dkt Matiang’i, Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Katibu katika Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa kufeli kuwasilisha Dkt Miguna kortini kulingana na maagizo ya mahakama.

“Mlalamishi anaomba kwamba Bunge la Kitaifa liwasilishe pendekezo kwa Mheshimiwa Rais kwamba Dkt Matiang’i afutwe kazi kama Waziri wa Usalama kwa kukiuka kiapo cha afisi, maadili ya kitaifa na kanuni za uongozi bora,” akasema.

Bw Sheikh anasema Dkt Miguna alifurushwa nchini mara mbili kwa sababu Dkt Matiang’i na maafisa walioko chini ya yake walikaidi maagizo ya mahakama.

Anataja maagizo yaliyotolewa na Majaji Luka Kimaru, Chacha Mwita na George Odunga kama ambayo Dkt Matiang’i na wenzake walikiuka na kupelekea kufurushwa kwa Dkt Miguna ambaye sasa amerejea Canada.

“Mnamo Machi 28, baada ya msururu wa ukiukaji maagizo ya mahakama, Jaji Odunga alimpata Dkt Matiang’i na hatia na kumwamuru, pamoja na maafisa wengine, alipe faini ya kima cha Sh200,00,” akasema kwenye ombi hilo lililopokewa rasmi na afisi ya karani wa Bunge la Kitaifa.