Habari Mseto

Mfanyabiashara akana kutoa hundi feki ya mamilioni

April 10th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa mnamo Jumanne, Aprili 9, 2024 kwa kulipa deni la Sh999,000 akitumia hundi akijua akaunti yake haikuwa na fedha miaka minane iliyopita.

John Malago Nderitu alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Samson Temu kwa kupeana hundi tatu mwaka wa 2016 akijua hana pesa zozote katika akaunti yake iliyokuwa kwenye Benki ya NIC.

Bw Nderitu alikana mnamo Aprili 16 , 2016 katika afisi za Granada Trading Company katika jengo la Twiga Towers Kaunti ya Nairobi alimwandikia Rajendra Sanghani hundi ya Sh999,000 akijua akaunti haikuwa na chochote.

Korti iliambiwa kwamba Bw Nderitu alikuwa ameandikia kampuni ya kuuza magari ya Subaru Motors Limited iliyokuwa imemwajiri Sanghani.

Shtaka la pili lilikuwa la kumpa tena

Sanghani hundi nyingine mnamo Aprili 26, 2016 akifahamu pia akaunti yake haikuwa na hela.

Mnamo Mei 17,2016 mshtakiwa alidaiwa kuandika hundi nyingine ya Sh999, 000.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “hatatoroka ila atafika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi.”

Bw Nderitu alimsihi hakimu amwachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu mno ikitiliwa maanani alikuwa nje kwa dhamana ya polisi ya Sh50, 000.

Upande wa mashtaka haukupinga akiachiliwa kwa dhamana.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh400, 000 na mdhamini mmoja wa kiasi hicho.

Hakimu pia alimpa dhamana mbadala ya Sh100, 000.

Kesi hiyo itatajwa tena mnamo Aprili 13, 2024 ili kutengewa siku ya kusikizwa.