Habari za Kitaifa

Mfanyabiashara akiri kumlawiti mwanamume mwenzake

March 15th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

MFANYIBIASHARA mmoja mwenye umri wa miaka 46 amekiri mbele ya mahakama ya Eldoret kwamba alimlawiti mwanamume mwenzake.

Patrick Imbali ambaye Ijumaa alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mwandamizi Richard Odenyo, alikiri kutenda kosa hilo huku akionekana kutoyumbishwa na hukumu inayomsubiri.

Nakala ya mashtaka ilisema kuwa Imbali alimlawiti F.K wa umri wa miaka 28 baina ya Machi 1 na Machi 13, 2024, katika mtaa wa Kambi Mwangi ulioko Turbo, viungani mwa mji wa Eldoret.

Licha ya kiongozi wa mashtaka kumuonya kuwa kosa ambalo alikiri lina adhabu kali, mshtakiwa alishikilia msimamo kwamba alimlawiti mlalamishi.

“Hakuna siri, ni kweli nilimlawiti mlalamishi na hata mimi najua tulifanya hiyo tabia,” akasema mshtakiwa.

Hata hivyo kiongozi wa mashtaka aliomba mahakama kumpa muda zaidi ili amsomee mshtakiwa maelezo ya mashtaka kwa kina.

“Kwa kuwa umekiri mashtaka, utazuiliwa katika rumande ya gereza kuu la Eldoret ukisubiri kurejeshwa mahakamani kusomewa maelezo ya mashtaka husika kama alivyoomba kiongozi wa mashtaka,” aliamuru hakimu Odenyo.

Katika mahakama iyo hiyo mwanamume mwingine alikiri kosa la kupatikana na misokoto 49 ya bangi na kuambia mahakama kuwa anatumia bangi hiyo kama dawa ya kumpa nguvu za kutekeleza majukumu yake kama mume nyumbani.

Benson Mwangi aliambia mahakama kwamba bangi aliyopatikana nayo si ya biashara.

“Ninatumia bangi kama dawa ya kuniongezea nguvu za kutekeleza majukumu kama mwanamume nyumbani miongoni mwa majukumu mengine yanayofaa kutekelezwa na wanaume katika jamii,” akasema Mwangi.

Kesi zote mbili zitatajwa Machi 22, 2024.