Mfanyabiashara anayeshtakiwa kujaribu kuua maafisa wawili wa polisi aachiliwa kwa dhamana ya Sh10milioni

Mfanyabiashara anayeshtakiwa kujaribu kuua maafisa wawili wa polisi aachiliwa kwa dhamana ya Sh10milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA anayeshtakiwa kwa kujaribu kuwaua maafisa wawili wa polisi aliachiliwa jana kwa dhamana ya Sh10milioni baada ya kukaa rumande kwa mwezi mmoja.

Bw Dickson Njanja Mararo aliachiliwa na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi Bi Esther Kimilu.Akimwachilia, Bi Kimilu alisema ni haki ya mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.

“Nimezingatia kwamba mshtakiwa amezuiliwa kwa siku 30 tangu akamatwe Julai 5, 2021 na kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Muthaiga na katika gereza la Viwandani,”Bi Kimilu alisema.Hakimu alisema licha ya upande wa mashtaka kusisitiza mshtakiwa anyimwe dhamana kwa vile mmoja wa maafisa aliyepigwa risasi angali hali mahututi “atamwachilia  kwa dhamana.”

Bi Kimilu alisema dhamana ni haki ya kila mshtakiwa kwa mujibu wa kifungu nambari 49 cha Katiba ya Kenya.Alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh10milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho au alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh5milioni.

Hakimu alitupilia mbali ombi la kiongozi wa mashtaka Bi Everlyne Onunga na wakili Daniel Maanzo anayewakilisha familia ya afisa wa polisi Festus Musyoka Kavuthi,mshtakiwa azuiliwe kwa mwezi mmoja.

Mawakili Cliff Ombeta (kushoto) anayemwakilisha Mararo na Bw Daniel Maanzo (kulia) anayewakilisha familia ya Festus Musyoka Kavuthi mmoja wa maafisa aliyejeruhiwa….Picha/RICHARD MUNGUTI

Bi Onunga na Bw Maanzo walieleza mahakama Bw Kavuthi angali hali mahututi na hajaandikisha taarifa ya ushahidi kwa afisa anayechunguza kesi hiyo.“Naomba hii mahakama isitishe uamuzi wa kumwachilia mshtakiwa kwa dhamana kwa vile mhasiriwa hajaandikisha taarifa kwa polisi jinsi aliumia,” Bi Onunga.

Kiongozi huyo wa mashtaka alidokeza tena “mhasiriwa huyo hajawahi zugumza kutokana na majeraha aliyopata shingoni.”Lakini wakili Cliff Ombeta anayemwakilisha mshtakiwa alipinga ombi hilo akisema “mshtakiwa hawezi kuzuiliwa hadi siku ile mhasiriwa atakapozugumza ambayo haijulikani ni lini.”

Bw Ombeta aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ikitiliwa maanani amezuiliwa kwa mwezi mmoja sasa.“Tangu mshtakiwa akamatwe yapata mwezi mmoja na inaaminika polisi wamekamilisha mahojiano na mashahidi,” Bw Ombeta.

Wakili huyo alisema anatumaini afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) imepata makao ya kuwahifadhi mashahidi wanaodaiwa wanahofia maisha yao.Mahakama ilikubaliana na Bw Ombeta kwamba lazima uchunguzi utiwe kikomo.

Mshtakiwa aliagizwa asiwavuruge mashahidi ama kutatiza sehemu iliyosalia ya uchunguzi.Bw Mararo amekanusha mashtaka matatu ya kujaribu kuwaua Bw Kavuthi, Bw Lawrence Muturi na weita katika hoteli ya Quiver iliyoko Kasarani Nairobi Felistus Nzisa mnamo Julai 2, 2021.

Bw Ombeta aliomba dhamana hiyo ya Sh10milioni ipunguzwe lakini Bi Kimilu akamweleza awasilishe ombi hilo Septemba 20, 2021 kesi itakaposikizwa.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ainua mikono

Wanafunzi 160 Githunguri wapata ufadhili wa Sh5 milioni