Habari za Kitaifa

Mfanyabiashara Deepak Kamani huru katika kesi ya sakata ya Sh7bn

January 19th, 2024 3 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA Deepak Kamani pamoja na nduguye Rashmi Kamani na makatibu wa zamani wa wizara Dave Mwangi, Joseph Magari, na Joseph Onyonka walipatikana bila hatia Ijumaa wakati hakimu Felix Kombo alitoa uamuzi wake katika kesi ya sakata ya Euro 40m (sawa na Sh7.05bn) za Anglo-Leasing.

Serikali kwa muda wa miongo miwili imekuwa ikijizatiti kuthibitisha kesi ya kashfa hiyo.

Lakini ilishindwa kabisa na wakenya wamepoteza mabilioni ya pesa wakisaka ukweli huku serikali ikijua kandarasi ya kuimarisha vyombo vya usalama iliyotia kati ya kampuni ya Sunday Day Corporation ilikuwa halali.

Wakili Edward Oonge aliyewatetea makatibu watatu wa zamani Mabw Onyonka, Mwangi na Mbui Magari walioshtakiwa pamoja wafanyabiashara wa kimataifa Deepak na nduguye Rashmi, alimweleza hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Kombo “wahasiriwa wa kesi hii ni wananchi wa Kenya waliopoteza mabilioni ya pesa huku serikali ikiandama kashfa ambayo haikuwa”.

“Serilali ilifukuza upepo na kusababisha mabilioni ya pesa za umma kupotea. Katika muda huu wote wa miaka 20 washtakiwa walisimamishwa kazi na kuendelea kupokea mishahara nusu, wachunguzi walitumia mamilioni ya pesa kusafiri hadi ng’ambo kusaka ukweli ilhali mradi wa kuboresha huduma za usalama kupitia ujenzi wa maabara kwa idara ya polisi ulikuwa halali. Mbona serikali iliamua kufukuza moshi?” Bw Oonge akasema na kuuliza huku akiipongeza mahakama kwa ‘kutenda haki’.

Wakili huyo alisema hayo baada ya hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi mahakama ya Milimani Felix Kombo “kuamua washtakiwa watano walioshtakiwa kwa kashfa hiyo hawana hatia.”

Akiwaachilia ndugu hao pamoja na waliokuwa makatibu wa wizara Mbw Mwangi (Masuala ya Usalama), Onyonka, Mbui Magari na aliyekuwa Waziri wa Fedha marehemu David Mwiraria, Bw Kombo alisema “kandarasi za kuuzia serikali silaha na kuboresha maabara ya idara ya polisi zilikuwa biashara halali na serikali ya Kenya ilifaa kulipia.”

Bw Kombo alisema zabuni iliyoipa kampuni ya ndugu hao pamoja na baba yao aliyekufa kabla ya kesi kukamilishwa iliidhinishwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Amos Wako.

Alisema hati za kandarasi hiyo ziliidhinishwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama Dkt Chris Murungaru wakati wa utawala wa hayati Mwai Kibaki.

Bw Kombo alisema mashahidi wote 37 waliofika mbele yake walieleza kuwa zabuni na kandarasi zilizosababisha kampuni ya Sunday Day Corporation ilikuwa halisi na kamwe hakukuwa na njama zozote za kuilaghai serikali ya Kenya mabilioni ya Kenya.

Hakimu aliwaachilia washtakiwa wote na kusema mashtaka saba ya kula njama ya kuilaghai serikali, kuwanufaisha Mabw Kamani na pesa za umma hayakuthibitishwa kamwe.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka nimefikia uamuzi washtakiwa wote watano walioko kizimbani hawakuhusika na ufisadi wowote,”alisema Bw Kombo.

Pia hakimu aliwakashfu maafisa wa polisi waliochunguza kesi hiyo kwa kutowashtaki wahusika wakuu waliojumuisha Dkt Murungaru ambaye alikuwa waziri wa usalama wakati huo 2003 na 2004.

Mahakama ilisema pia idara ya polisi ambayo ilikuwa inalengwa kufanikishwa haikushirikishwa wakati kandarasi hiyo ilipokuwa inaandaliwa.

Alisema aliyekuwa kamishna wa polisi Edwin Nyasenda hakuitwa kama shahidi pamoja na maafisa wakuu wengine serikali waliojua ukweli wa kandarasi hiyo.

Bw Kombo alisema kuwatowasilisha ushahidi wa wakuu hao waliohusika na usakaji na ufanikishaji wa kandarasi hiyo kulilemaza kesi ya upande wa mashtaka.

“Upande wa mashtaka ulidhani kutowaita utasaidia kesi waliyowasilisha kumbe waliiharibu,”Bw Kombo alisema akichambua ushahidi uliowasilishwa.

Mahakama ilisema kwamba kuwashtaki watano hao kulipelekea pesa za umma kupotea bure.

“Je kiini cha kuwasilisha kesi hii kilikuwa kipi ikitiliwa maanani Bw Wako ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali aliikagua zabuni na kusema ilikuwa halisi na halali?” Bw Kombo alishangaa.

Alisema wasimamizi wa idara ya usalama wa ndani haikuzingatia sheria kuwafungulia mashtaka washtakiwa.

Bw Kombo alisema: “Sina budi ila kuwaachilia washtakiwa kwa kukosekana ushahidi wa kuniwezesha kuwasukuma kizimbani kujitetea kwa kesi ya kula njama za kuilaghai serikali Euro 40 milioni.”

Hakimu huyo aliipa serikali muda wa siku 14 kukata rufaa.

Pia aliamuru dhamana walizoweka washtakiwa kortini warudishiwe.

Serikali iliwafungulia washtakiwa kesi mbili katika kashfa hiyo ya Anglo-Leasing na zote zimetupiliwa mbali.

Endapo washtakiwa wataishtaki serikali kulipwa fidia kwa kukamatwa na kushtakiwa bure, walipa ushuru watapoteza kiwango kikubwa cha pesa.