Habari Mseto

Mfanyabiashara kunaswa kwa kughushi hatimiliki

August 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA anayekabiliwa na  mashtaka ya kughushi hati za umiliki wa mashamba Jumatatu aliagizwa atiwe nguvuni.

Bw Patel Ravji Lalji aliagizwa akamatwe  alipokosa kufika kortini kujibu mashtaka saba dhidi yake.

Bw Lalji aliyeachiliwa Ijumaa kwa dhamana ya Sh30,000 na kuagizwa afike kortini Jumatatu hakufika hata ikabidi ombi la kukamatwa kwake likawasilishwa.

Kiongozi wa mashtaka Bi Angela Fuchaka aliomba mahakama itoe kibali cha kumtia nguvuni mshtakiwa “ kwa kutotii agizo la polisi afike kortini Jumatatu kujibu shtaka.”

“Naomba hii mahakama itoe kibali cha kumtia nguvuni mshtakiwa. Alikaidi hii mahakama.Alidharau agizo afike kortini kujibu shtaka.”

Mshtakiwa alikuwa amepewa dhamana ya polisi ya Sh30,000.

Kwa mujibu wa hati za mashtaka Bw Lalji alighushi hati ya mauzo ya shamba akidai limetiwa sahini na Bi Helen Odhiambo Oburu.

Pia alikabiliwa na shtaka la kughushi hati za kuidhinisha malipo 42 akidai zimetiwa sahini na Bw Hezbon Omondi.

Mshukiwa huyo anakabiliwa na shtaka lingine la kughushi hati akidai zimetiwa sahini na kampuni ya mawakili ya Nikitta Akinyi, Okundi Ogonji.

Pia alidaiwa alighushi hati nyingine  akidai imeidhinishwa na  kampuni ya mawakili ya Odhiambo Oburu,Akinyi & Ogonji Advocates

Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi aliagiza kesi itajwe Jumatano.