Habari

Mfanyabiashara Nginyo Kariuki azikwa Tigoni

March 3rd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amemsifu mwanasiasa na mfanyabiashara Nginyo Kariuki kama mtu shupavu ambaye wakati wa uhai wake alikuwa na bidii na mshauri mwenye tajriba kubwa.

Kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki wakati wa mazishi ya Mzee Kariuki, Rais alisema taifa hili litakosa mchango wa marehemu ambaye aliwekeza kwa ajili ya kuboresha jamii.

“Mzee Nginyo Kariuki alikuwa ni kiongozi ambaye aliwasaidia wengi maishani mwake. Hii ni kutokana na weledi wake katika nyanja za siasa na biashara. Aliwekeza katika jamii,” Rais akasema.

Bw Kihara alisema kiongozi wa taifa alikuwa amepanga kuhudhuria mazishi hayo katika eneo la Tigoni lakini hangeweza kufika kutoka na mkutano wa dharura ambayo alitarajiwa kuongozo kuhusu kero la virusi vya corona.

“Rais alikuwa amevalia kwa ajili ya kujumuika nanyi kumuaga rafiki yake lakini akabanwa na shughuli za kiserikali,” akasema Bw Kariuki.

Kwa upande wake, kiongozi wa ODM Raila Odinga amemtaja marehemu Nginyo kama mtu ambaye alipata mali yake kisheria na kwa njia ya uwazi.

“Nginyo ndiye mtu ambaye alifaa kutajwa kwa “hasla kamili”.

Nyakati zote alikuwa mtu mwadilifu na ambaye alipata mali yake kwa kihalali.

Bw Odinga amefichua kwamba marehemu Nginyo ndiye mmoja wa wanasiasa walioongoza juhudi za maridhiano kati yake na Rais Kenyatta baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Wanafamilia na marafiki wabeba jeneza la mfanyabiashara Nginyo Kariuki wakati wa mazishi yake eneo la Tigoni, Kaunti ya Kiambu Machi 3, 2020. Picha/ Simon Ciuri

“Nginyo alikuja mara kadha nyumbani kwangu Bondo kwa ajili ya kuleta maridhiano kati yangu na Rais. Wakati mmoja aliandamana na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria. Nadhani alitumia wakati huo kumfundisha Kuria maadili mema,” ameeleza.

Bw Odinga amewashambulia mahasidi wake wa kisiasa akisema kwa kuiga maisha ya marehemu Nginyo, viongozi wakome kubeba pesa kwa magunia na kuzisambaza katika mikutano ya harambee bila kueleza chanzo cha mapato yao.

Akasema: “Tunataka kupambana na saratani ya ufisadi. Hufai kutembea na magunia ya pesa kupeleka kwa harambee na kudai unawekeza mbinguni. Tunataka uwekeze hapa duniani alivyofanya marehemu Nginyo.”

Huku akimtaja marehemu kama mpiganiaji shupavu wa kurejelewa kwa demokrasia ya vyama vingi nchini, Bw Odinga amekariri kujitolea kwa kulinda utawala huo kuwa kuendelea na juhudi za kuunganisha taifa hili.

Mazishi hayo pia yamehudhuriwa na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, Seneta wa Siaya James Orengo na wengineo.

Wote waliohutubu wamemmiminia sifa marehemu Nginyo ambaye pia alikuwa mchezaji gofu mashuhuri.