Habari

Mfanyabiashara wa Mombasa anaswa kwa kukwepa ushuru

September 6th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) na Idara ya Upelekezi wa Jinai (DCI) Ijumaa zimeendeleza operesheni za kuwaandama wakwepaji ushuru nchini.

Wa hivi punde kukamatwa kwa kosa hilo ni mfanyabiashara wa Mombasa Bw Abdi Gedi Amini. Alikamatwa Alhamisi mjini Mombasa kwa kuhusika katika mtandao wa ukwepaji ushuru unaofikia kiasi cha zaidi ya Sh1 bilioni.

Anatarajiwa kufikishwa mahakamani Ijumaa alasiri kufunguliwa mshtaka ya kukwepa kulipa ushuru, kudinda kuwasilisha ripoti yake ya ulipaji ushuru na kutoa habari ya uongo inayoathiri wajibu wake na kampuni zake kulipa ushuru.

Makosa hayo yanakwenda kinyume na sehemu ya 97 (c) ikisomwa pamoja na sehemu ya 104 (3) ya Sheria kuhusu Utaratibu wa Ulipaji Ushuru ya 2015.

Kwenye taarifa iliyotumwa vyombo vya habari Ijumaa KRA imesema kwamba Bw Abdi anadaiwa kuunda kampuni saba ambapo ama yeye ni mkurugenzi au anatumia washirika wake kuziendesha.

Usemi

Washirika hao pia ndio wenye usemi katika akaunti za kampuni hizo katika benki (bank account signatories).

Kampuni hizo zimekuwa zikiendesha biashara za utengenezaji bidhaa, uuzaji bidhaa kwa jumla na rejareja (bidhaa kama sukari, mafuta, na zile ndogo ndogo) na biashara ya kutoa huduma za uchukuzi.

Kampuni hizo zinaendesha shughuli katika Kaunti za Mombasa na Nairobi.