Habari Mseto

Mfanyakazi mochari aambia mahakama marehemu Mwingereza hakuwa na msokoto wa bangi

December 3rd, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO na BRIAN OCHARO

MFANYAKAZI katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali binafsi ya Pandya ambako mwili wa raia wa Uingereza Alexander Monson ulipelekwa baada ya kufariki katika hali ya kutatanisha mikononi mwa maafisa wa polisi adai kuwa mwendazake hakupatikana na chochote kama walivyodai polisi.

Kauli ya mfanyakazi huyo Bw Chelestino Ngari imekinzana na ile ya maafisa wanne wa polisi wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Monsoon, ambao walidai kuwa mwendazake alipatikana na msokoto wa bangi katika nguo zake.

Maafisa hao John Pamba, Naftali Chege, Charles Wang’ombe Munyiri, na Ishmael Baraka Bulima walikanusha kumuua Monsoon miaka saba iliyopita wakidai kuwa alifariki baada ya kutumia madawa ya kulevya kupita kiasi.

Hata hivyo, Bw Ngari akitoa ushahidi mbele ya Jaji Erick Ogolla amesema hawakupata kitu chochote kwenye nguo za marehemu walipokuwa wanamvua nguo marehemu kwa harakati za upasuaji mwili kwa uchunguzi.

“Tulitafuta katika mifuko na nguo za marehemu kwa jumla lakini hatukupata kitu; shughuli hiyo ilishuhudiwa na afisa mmoja wa usalama, mpasuaji wa serikali na raia mmoja wa Uingereza,” shahidi huyo ameeleza mahakama.

Baada ya upasuaji mfanyakazi huyo ameeleza kuwa alichukuwa sampuli za mikojo, ini, matumbo na vitu vingine kumpelekea mchunguzi wa maiti.

“Maafisa wa polisi pia walichukua baadhi ya viungo kutoka kwa mwili wa mwendazake kupeleka katika maabara ya serikali,” ameeleza.

Aidha amedai raia wa kigeni aliyekuwa anafuatilia kwa karibu uchunguzi wa maiti pia alichukua baadhi ya viungo japo ni kinyume cha sheria. Taifa Leo haiwezi kuthibitisha dai hilo.

“Maafisa wa usalama pekee na mamlaka huru huruhusiwa lakini si raia wa kawaida,” amesema.

Kulingana na maelezo yaliyowasilishwa mahakamani, inadaiwa maafisa hao walimuua Monson mnamo Mei 18-19 mwaka 2012 eneo la Diani, Kaunti ya Kwale.

Mwanzoni mwa kesi Afisa wa polisi William Serem ambaye alimkamata Mwingereza huyo eneo moja Diani, alisema kuwa marehemu alikuwa katika hali nzuri ya afya.

Walimkamata kwa madai kuwa alipatikana na misokoto ya bangi.

Aidha alieleza mahakama kuwa marehemu alipokuwa chini ya uangalizi wake alikuwa salama na hata alikuwa akitetea watu wengine aliokamatwa nao.

“Walipokuwa wanaandikishwa katika meza ya usajili Monson ambapo aliwaamrisha maafisa wa polisi kumuachilia baadhi waliokuwa wamekamatwa pamoja naye akidai kuwa hakuhusika na bangi iliyopatikana,” akaeleza Serem.

Kesi itaendelea Jumatano.