Habari Mseto

Mfanyakazi wa kaunti akana kuwalaghai wakazi wa jiji Sh5.5 milioni

February 13th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYAKAZI wa kaunti ya Nairobi Jumatatu alishtakiwa kwa kufanya njama za kuwalaghai wananchi zaidi ya Sh5.5 milioni akiwadanganya atawasaidia kupata leseni za kuendeleza biashara jijini.

Claire Munde Omufwoko alikana mashtaka mawili dhidi yake mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot.

Omufwoko alishtakiwa kutekeleza ulaghai huo katika afisi ya fedha iliyoko City Hall. Pia alikana aliiiba Sh1,550,000.

“Naomba hii mahakama izingatie mshtakiwa ameifanyia NCC kwa miaka 29. Mwachilie kwa kiwango kisicho cha juu cha dhamana,” wakili Anne Nderu anayemwakilisha mshtakiwa alimsihi hakimu.

Kesi dhidi ya Omufwoko itaunganishwa na nyingine dhidi ya washtakiwa wengine ambao wako nje kwa dhamana ya Sh400,000.

Kesi hiyo itasikizwa Machi 12. Bw Cheruiyot alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh30,000.

Kesi iliongozwa na Bi Cynthia Opiyo.