Habari Mseto

Mfanyakazi wa Khalwale kuzikwa Jumatatu

February 3rd, 2024 2 min read

NA SHABAN MAKOKHA

KIZITO Amukune Moi, mwanaume ambaye alidungwa kwa pembe na fahali wa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, atazikwa mnamo Jumatatu.

Hii ni baada ya ripoti ya upasuaji wa maiti kuthibitisha kuwa mfanyakazi huyo alikufa kutokana na majeraha ya kudungwa kwa pembe ya fahali huyo, Inasio.

Mazishi yake awali yalikuwa yameratibiwa yafanyike mnamo Januari 30 lakini yakaahirishwa baada ya madai na utata kuzuka kuhusu mauti yake.

Upasuaji uliofanywa na Dkt Dickson Muchana ulionyesha kuwa mfanyakazi huyo wa Dkt Khalwale aliaga dunia kutokana na majeraha aliyosababishiwa na fahali huyo.

Polisi kutoka Ikolomani walisimamisha mazishi hayo kupisha uchunguzi zaidi wa maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na pia ufanyiwe upasuaji kwa mara ya pili kubaini kilichosababisha mauti yake.

Makachero hao wa DCI waliwasili Kakamega mnamo Ijumaa  asubuhi na kukita kambi nyumbani kwa Bw Khalwale  wakifanya uchunguzi wao. Baadaye waliungana na Mwanapatholojia wa serikali Dkt Johansen Oduor kwa uchunguzi wa postmortem katika Chumba cha Kuhifadhi maiti cha  Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega mnamo Jumamosi.

Dkt Oduor alithibitisha kuwa matokeo ya pili ya uchunguzi wa postmortem yalithibitisha yale ya kwanza.

“Tulifanya upasuaji kwa mara ya pili baada ya ule wa kwanza kutokubalika. Mwili ulikuwa na majeraha ya ndani ambayo  yalisababishwa na kifaa butu na kuashiria pembe ya mnyama,” akasema Dkt Oduor.

Kwa mujibu wa Dkt Oduor, mwili ulikuwa na majeraha kichwani upande wa kulia, shingoni na ndani ya mapaja.

“Matokeo haya yanaonyesha kuwa uchunguzi wa kwanza ulikuwa sawa. Mauaji hayo yalisababishwa na mnyama na ni kinyume cha madai kuwa alidungwa kisu,” akaongeza Dkt Oduor.

Dkt Khalwale alisema matokeo hayo yameiondolea familia yake madai yaliyokuwa yakienezwa mitandaoni kuwa marehemu aliuawa kwa kudungwa kisu.

“Nawashukuru maafisa wa DCI wa kutoka kwa ofisi za viwango vyote ikiwemo ya eneo hili na mwanapatholojia wa serikali kwa kuweka zingatio katika suala hili. Ukweli umebainika na sasa umetenganishwa na uongo,” akasema.

Alisema familia ya marehemu na vijana ambao huongoza hafla za kupigana kwa mafahali na wanakijiji wa Malinya, watachukua mwili huo kutoka mochari Jumapili na mazishi yatafanyika mnamo Jumatatu.