Habari za Kitaifa

Mfugaji atoa ng’ombe kumtuza Rais Ruto kwa kuiletea Kenya mazuri

May 28th, 2024 1 min read

NA OSBORN MANYENGO

MFUGAJI mmoja kutoka kijiji cha Huruma eneobunge la Cherangany, ametoa ng’ombe wake kwa lengo la kumtuza Rais William Ruto, kufuatia mafanikio makubwa aliyopata kwenye ziara yake rasmi nchini Amerika.

Akiwahutubia wanahabari nyumbani mnamo Jumanne, Bi Ruth Manaseh, alisema lengo la kumpa Rais Ruto zawadi hiyo ya ng’ombe ni kumrudishia shukurani kwa matunda tele ambayo alipata alipokaribishwa na Rais wa Amerika Joe Biden.

Kenya ilifanywa Mshirika wa Karibu wa Amerika asiyekuwa mwanachama wa kundi la kujihami la Nato. Ushirikiano huu unainua hadhi ya Kenya ambapo ni kumaanisha uwezo wa wanajeshi wa Kenya (KDF) unatambulika na mataifa yenye nguvu duniani.

Aidha Kenya ilituzwa helikopta 16 za kijeshi na ikapata dili nzuri ya magari ya kivita 150.

Mafanikio hayo miongoni mwa mengine yamefanya Bi Manaseh kuwakosoa vikali wale ambao wanaisuta serikali wakidai ujumbe wa Rais Ruto ulitumia pesa nyingi za mlipa ushuru kwenye ziara hiyo.

Aliwataka wakosoaji kwanza waangalie mafanikio ya hiyo safari.

Alitoa pia mfano wa msaada wa kuiwezesha Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutekeleza majukumu yake kufanikisha demokrasia na ushirikiano wa kuipiga jeki Wizara ya Afya kuwa ni miongoni mwa mafanikio hayo.

“Kwanza natoa shukrani zangu kwa Rais Ruto kwa ziara yake ya Amerika ambapo bila shaka alienda kutafutia watoto wake. Kwa kweli imezaa matunda na ndio sababu nimeamua kutoa ng’ombe wangu wa miezi 16 kama zawadi ya kumshukuru. Hakuna kingine ninachohitaji bali ni kumshukuru tu,” akasema Bi Manaseh ambaye pia hufuga kuku wa kienyeji, na nguruwe.

Mbali na ufugaji, Bi Manaseh pia ni mkulima anayepanda ndizi.

Alitoa wito kwa viongozi waliochaguliwa kushirikiana na Rais kwa lengo la kuboresha uchumi wa nchi badala ya siasa za kupigana vita na kujipima kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.