Akili MaliMakala

Mfugaji wa ng’ombe wa maziwa kidijitali

Na SAMMY WAWERU July 9th, 2024 2 min read

KATIKA kijiji cha Ondiri, Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, kwenye boma la John Makumi tunakaribishwa na milio ya ng’ombe. 

Ukiwa mwendo wa kumi hivi za jioni, sauti za ng’ombe waliokomaa na ndama zinahinikiza anga.

Tunampata akikama maziwa, wanaozalisha wakiwa zaidi ya watatu.

Kila ng’ombe, inamchukua karibu dakika kumi kukama huku wakiendelea kujienjoi na mlo kuwatuliza.

Makumi anadokeza kwamba amekuwa kwenye ufugaji tangu 2018.

“Nilianza na ng’ombe mmoja, na kufikia 2020 idadi ilikuwa imeongezeka hadi watatu,” anasema.

John Makumi mfugaji eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu akikama ng’ombe maziwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Huku ukulima na ufugaji ukihitaji maarifa kuufanikisha, Makumi anasema alihangaishwa na maradhi ya mifugo.

Anataja Kititi, maarufu kama Mastitis kwa lugha ya Kiingereza, kama mojawapo ya magonjwa yaliyomtatiza.

Ni ugonjwa unaosababisha titi au matiti ya ng’ombe kuvimba, wakiishia kutoa maziwa ya rangi ya manjano.

“Kimsingi, ni maradhi yanayochochewa na uchafu kwenye zizi la ng’ombe na jinsi ya kuwatunza,” asema.

Mwaka huohuo wa 2020, mradi wake ulipoanza kupanuka ndipo alipofunguka macho jinsi ya kupambana na changamoto zilizomzingira.

John Makumi akielezea safari yake katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kijiji cha Ondiri, Kikuyu, Kaunti ya Kiambu.

Kulingana na Makumi, ni kupitia apu ya DigiCow alianza kunoa makali kuhusu ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa na kuuendeleza kitaalamu.

Ni apu ya kidijitali inayotoa mafunzo ya ufugaji wa ng’ombe hasa wa maziwa yanayojumuisha; malisho yaliyoafikia ubora wa bidhaa za mifugo, bridi za ng’ombe waliopo Kenya, uzalishaji maziwa, afya ya mifugo, na mbegu za kisasa kutungishaji ujauzito – AI (Uhamilishaji).

“Ni apu ya simu na mtumizi – mfugaji huitoa kwenye Playstore. Mafunzo huyatoa kwa kutumia kanda za sauti na video kupitia wataalamu na wafugaji waliobobea,” anaelezea Jemimah Wanjiku, mmoja wa waasisi wa DigiCow.

Apu ya DigiCow kuendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, apu hiyo yenye zaidi ya wakulima 60, 000 ina jukwaa la kuunganisha wakulima na wataalamu wa mifugo, wakiwemo mavetinari walioidhinishwa na Bodi ya Huduma za Vetinari Kenya (KVB).

Anachohitaji mtumizi ni kuwa na data pekee, kwani hakuna ada au malipo anayotozwa kujiandikisha.

Makumi anaambia Akilimali kwamba ni kupitia huduma hizo za kidijitali aliweza kuboresha ufugaji wake.

“Kwa sasa, kero ya kukosa daktari (vetinari) imekuwa historia. Huwapata kupitia apu ya DigiCow. Isitoshe mtandao huo ndio taasisi yangu kujielimisha kuhusu uundaji chakula na kutangamana na wafugaji wengine waliobobea,” afafanua.

Shukran kwa mtandao huo, akikumbuka siku ambayo nusra apoteze ng’ombe wake kwa sababu ya ugonjwa hatari wa Kititi.

Miaka minne baada ya kukumbatia mfumo huo wa kisasa kunoa makali ya ufugaji, Makumi anakiri kuwa na kila sababu ya kutabasamu.

Jemimah Wanjiku, mmoja wa waanzilishi wa apu ya DigiCow kusaidia wafugaji kuboresha huduma. PICHA|SAMMY WAWERU

“Kutoka uzalishaji wa chini ya lita 10 kwa siku kwa kila ng’ombe, sasa ninachezea wastani wa 20.”

Isitoshe, ni kupitia apu hiyo alifanikiwa kujiunga na Kikuyu Dairy Cooperative, chama cha ushirika eneobunge la Kikuyu kinachosaidia wafugaji kupata soko la maziwa lenye ushindani mkuu.

Anafichua kuwa lita moja hununuliwa Sh49.

Apu ya DigiCow ilianzishwa 2016, Jemimah Wanjiku akisema kando na huduma za ufugaji bora wanazotoa, pia huelimisha wakulima jinsi ya kuweka rekodi.

“Mtandao wenyewe unashirikisha huduma zote za ufugaji, ikiwemo sehemu ya mkulima kusajili idadi ya ng’ombe alionao, kiwango cha uzalishaji maziwa, rekodi ya matibabu, chakula, uuzaji, afya, na mengineyo,” Wanjiku anaelezea.

Huhudumu kwa karibu na Idara ya Ufugaji, Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro), kati ya wadauhusika wengine kwenye utandawazi wa ufugaji.

Ng’ombe wa John Makumi ambaye ni mfugaji Kiambu huzalisha wastani wa lita 20 kila moja. PICHA|SAMMY WAWERU