Mfumaji Mason Greenwood ajiondoa kwenye timu ya taifa ya Uingereza kutokana na jeraha

Mfumaji Mason Greenwood ajiondoa kwenye timu ya taifa ya Uingereza kutokana na jeraha

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Manchester United Mason Greenwood amejiondoa katika timu ya taifa ya Uingereza inayojiandaa kwa fainali zijazo za Euro kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021 kwa sababu ya jeraha la paja.

Greenwood, 19, alitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi ambacho kingetegemewa na kocha Gareth Southgate kwenye kampeni hizo za Euro. Hata hivyo, Man-United wamefichua kwamba sogora huyo atasalia uwanjani Old Trafford ili jeraha lake litathminiwe zaidi.

Licha ya kujivunia ufufuo wa makali yake, fowadi wa Man-United, Jesse Lingard ametemwa kwenye kikosi cha Uingereza.

Lingard, 28, aliridhisha sana katika kikosi cha West Ham alichokuwa akichezea kwa mkopo kutoka Man-United msimu huu wa 2020-21. Alifunga jumla ya mabao tisa na kuchangia matano mengine kutokana na mechi 16 ligini.

Southgate anatarajiwa kufichua kikosi chake cha mwisho cha wanasoka 26 watakaoshiriki Euro katika tukio litakalomshuhudia akitema wachezaji sita zaidi kutoka timu ya sasa ya wachezaji 32.

Greenwood aliwajibishwa mara 52 katika mapambano mbalimbali ya Man-United mnamo 2020-21 na akafunga mabao 12. Ufanisi huo ulisaidia Man-United kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kutinga fainali ya Europa League.

Greenwood alichezea Uingereza kwa mara ya kwanza kwenye gozi la UEFA Nations League mnmoa Septemba 2020 dhidi ya Iceland.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Covid-19: Raila atoa wito serikali izindue miradi mingi...

Vita vya Uhuru na mahakama vingalipo