Makala

Mfumo kubaini mbegu halali, vita dhidi ya matapeli vikiendelea 

January 29th, 2024 2 min read

VITALIS KIMUTAI na SAMMY WAWERU 

WAFANYABIASHARA wanne wamekamatwa kwa madai ya kuuza mbegu bandia kwa wakulima Kaunti ya Kericho.

Shirika la Kutathmini Ubora wa Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis), liliendesha oparesheni kwa ushirikiano na maafisa wa polisi na kukamata wafanyabiashara hao.

Kukamatwa kwao kulijiri wakati wakulima wamekuwa wakilalamikia mimea yao kuvamiwa na wadudu na magonjwa mbalimbali ukanda wa Kusini mwa Bonde la Ufa.

Wakulima wakionyesha pakiti za mbegu zenye lebo ya Kephis. PICHA|SAMMY WAWERU

Washukiwa hao walikamatwa siku chache tu baada ya wafanyabiashara wengine sita kunyakwa Kaunti ya Bomet kwa kuuza mbegu ambazo hazijaidhinishwa na Kephis.

Uuzaji wa mbegu feki umekuwa na mchango hasi kwa nia ya serikali ya kuongeza mavuno kupitia mpango wa kusambaza mbolea ya bei nafuu. Mpango huo ambao umekuwa ukiendelea kwa mwaka moja na nusu, ulilenga kuhakikisha kuwa serikali inapunguza chakula kinachoagizwa kutoka nje ya nchi.

“Baadhi ya wafanyabiashara walikamatwa baada ya kupatikana wakiuza mbegu feki. Mbegu hizo hazikupakiwa na zilikuwa zikiuzwa eneo la wazi na pia hazikuwa na nembo ya Kephis,” akasema mmoja wa wakurugenzi wa Kephis Simeon Main.

Bw Maina ambaye anasimamia idara ya mauzo ya mbegu alisema kuwa wengi wa wafanyabiashara wenye maduka ya kuuza mbegu nao hawana leseni ya Kephis.

Pakiti ya mbegu yenye stika ya Kephis. PICHA|SAMMY WAWERU

“Tunawaomba wakulima wahakikishe kuwa wamenunua mbegu ambazo zimeidhinishwa ili kuepuka hali ambapo wanauziwa mbegu feki,” akasema Bw Maina.

Mwaka 2017, Kephis kwa ushirikiano na kampuni na mashirika ya pembejeo, ilizindua mfumo wa lebo na stika kubaini uhalisia wa mbegu.

Kupitia teknolojia hiyo, mkulima anatakiwa kukwaruza lebo yenye nembo ya Kephis na kutuma nambari za usajili za pakiti yenye mbegu kwa namba zilizotolewa na taasisi hiyo ya kiserikali kubaini ikiwa ni halali au feki.

Antonina Kandie, afisa kutoka Kenya Seed akionyesha pakiti yenye nembo na stika ya Kephis kubaini uhalisia wa mbegu. PICHA|SAMMY WAWERU

Stika hiyo ni sheria kwa mashirika na kampuni zote zinazounda na kuuza mbegu nchini.

Aidha, kampuni za mbegu zimeletwa pamoja kupitia Muungano wa Waundaji Mbegu Kenya (STAK), unaoshirikisha asasi za kiserikali na kibinafsi.

Mwaka uliopita, muungano huo uliandikisha visa vitatu vya wauzaji wa mbegu bandia.

STAK inapendekeza adhabu kali kwa wahusika.