Mfumo mbadala wasaidia KRA kukusanya Sh21 bilioni

Mfumo mbadala wasaidia KRA kukusanya Sh21 bilioni

Na BENSON MATHEKA

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA), imekusanya zaidi ya Sh21 bilioni kupitia mfumo mbadala wa kutatua mizozo inayohusu kodi (ADR) ulioanzishwa 2015.

KRA inasema kwamba mfumo huo umewezesha kutatuliwa kwa kesi 393 kati ya Julai 2020 na Machi 2021 ambazo zingechukua muda mrefu iwapo zingefuata mfumo wa kawaida wa kusikilizwa kortini.

KRA ilisema kwamba idadi ya kesi zilizotatuliwa kupitia mfumo huo iliongezeka kwa asilimia 109 na pesa zilizokusanywa zikaongezeka kwa asilimia 389 katika kipindi cha miezi tisa ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka wa kifedha wa 2019/ 2020.

Kulingana na sheria ya kodi, mizozo inayotatuliwa kupitia ADR inafaa kuchukua siku 90 japo baadhi imekuwa ikichukua siku chache.

“Licha ya changamoto za sasa za janga la corona, utatuzi wa mizozo kupitia ADR umeendelea bila kukwama kwa kuwa mikutano inafanywa kwa video. Hii pia imepunguza muda ambao mikutano hufanyika,” KRA ilieleza.

Mamlaka hiyo ilipongeza mfumo huo ikisema unadumisha uhusiano kati yake wa mlipa ushuru.

“Mpatanishi huwa anahakikisha kwamba pande zote zinadumisha uhusiano mwema. Hii hufanya kila upande kuwa mshindi,” KRA ilieleza kwenye taarifa.

ADR huwa unapunguza muda na gharama ya kuwasilisha kesi kortini na hivyo kuokoa pesa.

You can share this post!

Mkanganyiko mkuu unavyogubika siasa za urithi Pwani

CHOCHEO: Jifunze kuomba msamaha ili furaha irejee kwenye...