Habari Mseto

Mfumo mpya wa ugavi wa fedha za kaunti

December 19th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Ugavi wa Rasilimali (CRA) imependekeza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti uongezwe kutoka Sh314 bilioni hadi Sh335 bilioni katika mwaka wa kifedha ujao wa 2019/2020.

Tume hiyo pia imependekeza utaratibu mpya wa utakaotumiwa katika ugavi wa fedha hizo ambapo serikali za kaunti ambazo zitakusanya fedha nyingi na kudumisha usimamizi mzuri wa rasilimali za umma zitapokea kiasi kikubwa cha fedha hizo katika kipindi hicho cha matumizi ya Sh335 bilioni zilizopendekezwa kugawanywa miongoni mwazo katika mwaka ujao wa kifedha.

“Fedha hizo pia zitagawanywa kwa misingi ya mahitaji ya sekta mbalimbali katika serikali hizo huku sekta ya afya ikitengewa asilimia 15 ya mgao wa fedha katika kila kaunti. Kiasi hicho ni sawa na Sh1,035 kwa kila mwananchi asiyekuwa na bima ya matibabu,” akasema mwenyekiti wa tume hiyo Jane Kiringai kwenye kikao na wanahabari Jumanne jijini Nairobi.

Utaratibu huo mpya utatumika pamoja na ule wa zamani uliozingatia masuala kama vile; Idadi ya Watu, Ugavi sawa, Umasikini, Ukubwa wa Kieneo, Majukumu ya Kifedha na Kiwango cha Maendeleo.

Dkt Kirinngai alisema utaratibu huo mpya ugavi wa fedha kwa kaunti unalenga kuhakikisha kuwa ugatuzi unawanufaisha wananchi katika maeneo ya mashinani kwa kukoleza falsafa ya matumizi ya usimamizi mzuri wa kifedha za umma.

“Hii ni maana kama tume tunalenga kuzizawadia kaunti ambazo zitakumbatia matumizi mazuri ya fedha za umma bila kuzingatia bajeti zao na idadi ya watu,” akasema.

“Hii ndio maana vile vile, tunapendekeza kuwa kaunti ambazo zitakusanya fedha nyingi zitapata mgao wa juu kuliko zile ambazo zitazembea katika nyanja hii,” akaongeza.

Dkt Kiringai alisisitiza kuwa zile serikali ambazo zitaruhusu wizi au ubadhirifu wa fedha za umma kunawiri hazitapunguziwa kiwango cha mgao.

Hata hivyo, Dkt Kiringai alisema hayo ni mapendekezo ya tume yake na yatahitaji kuidhinishwa na Seneti mapema mwaka ujao kabla ya kuanzia kuanzia kutumika.

“Vigezo hivi vipya ambavyo vinaunda msingi wa tatu wa ugavi wa fedha kwa kaunti bado vitajadiliwa na Maseneta. Vile vile, tume hii itaendesha vikao kote nchini ambapo wananchi wataruhusiwa kutoa maoni au mapendekezo yao kuvihusu,” akafafanua.

Dkt Karinga, ambaye alikuwa ameandamana na makamishna wote wa tume hiyo, alisema pia alisema kuwa utaratibu huo mpya umependekezwa kufuatia malalamishi yaliyotolewa kuhusu utaratibu ambao umekuwa ukitumika tangu 2013.

“Tunaamini kuwa utaratibu huu mpya tuliopendekeza utajibu maswali yaliyoibuliwa kuhusu ule wa zamani ambapo ilidaiwa ugavi wa fedha hizo haukuzingatia usawa. Kwa mfano, ilidaiwa kuwa kaunti kama Lamu ilipata fedha nyingi kwa misingi ya kuwa na idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na Nairobi, au Kiambu zenye watu wengi,” akasema.

Mwenyekiti huyo, hata hivyo, alisema katika utaratibu wa sasa kigezo cha idadi ya watu kitachukua asilimia 45 ya fedha, ugavi sawa (asilimia 26), umasikini (asilimia 18), ukubwa kieneo (asilimia 8) na usimamizi wa kifedha (asilimia 2).

Chini ya utaratibu huu kaunti ya Nairobi ndio itapata kiwango cha juu zaidi cha mgao katika mwaka ujao wa kifedha wa 2019/2020, kwa kutengewa Sh17,440. Kaunti ya Lamu nayo itapokea mgao wa chini kabisa wa Sh2,463.