Mfumo wa haki wa kitamaduni waokoa kaka walioua jamaa

Mfumo wa haki wa kitamaduni waokoa kaka walioua jamaa

Na PHILIP MUYANGA

MFUMO wa haki wa kitamaduni umetumiwa kuwatetea kaka wawili walioua jamaa wa familia yao kufuatia mzozo kuhusu kisima cha kunywesha mifugo wakafungwa kifungo cha nje cha miaka mitatu kwa kuua bila kukusudia.

Jaji Roseline Korir alikubali ripoti ya maafisa wa probesheni kwamba kupitia mfumo huo, washtakiwa Guyo Uren na kaka yake Musa Hurrein walijuta kwa kitendo chao na kwamba familia yao ilikuwa imepatana na ya mwathiriwa na kurejesha amani katika jamii.

“Katika hali hii basi, mfumo wa haki wa kitamaduni unaweza kusemekana kuwa utetezi unaofaa kuzingatiwa na mahakama na kutoa makali ya adhabu,” alisema Jaji Korir. Kaka hao wawili walishtakiwa Juni 13, 2017 katika Mahakama Kuu ya Garsen kwa kumuua Osman Boba. Walikiri mashtaka lakini baadaye wakakubaliana na upande wa mashtaka kushtakiwa kwa kosa dogo la kuua bila kukusudia.

Ripoti ya afisa wa probesheni ilisema kuwa familia ya washtakiwa na ya marehemu zilikuwa zinajuana na zina uhusiano wa kindoa. Ripoti inasema kisa hicho kilizua uhasama kati ya familia hizo mbili na kila moja ikaondoa binti yao aliyeolewa katika familia nyingine.

Mahakama iliambiwa baraza la wazee wa Orma (Matadeda) waliamua kwamba familia ya washtakiwa ihame kutoka Waldena hadi Assa Kone; na familia ya mwathiriwa ifidiwe ng’ombe 70, idadi iliyopunguzwa hadi 48.

Ripoti ilisema baada ya familia ya marehemu kupata ng’ombe hao 48, ilirejesha kwa hiari, ng’ombe wanne na familia zote mbili zikasameheana bila masharti zaidi na ile ya washtakiwa ikapokelewa katika jamii.

Mahakama iliambiwa familia zote mbili hazina uhasama tena na washtakiwa hawakupinga adhabu yoyote nafuu ambayo mahakama ingewapa. Jaji Korir alisema baada ya kuzingatia lengo la hukumu, utetezi na pia taarifa ya athari kwa upande wa waathiriwa, alishawishika kuwapa washtakiwa kifungo cha nje.

  • Tags

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Mahaba ya video yanitosha’

Mfumo mpya wa wasaka-kazi kuwafaa vijana