Habari za Kitaifa

Mfumo wa Ufadhili: Wanachuo wakemea rais kwa kinywa kipana


IKULU ilitumia takriban Sh3 milioni kupanga mkutano ambao ulinuiwa kuwashawishi viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu kuidhinisha mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu.

Hata hivyo, mkutano huo haukumalizika vizuri, kwa kuwa malalamishi ya wanafunzi hayakushughulikiwa kikamilifu.

Takriban viongozi 100 wa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali kote nchini walihudhuria mkutano huo uliochukua saa tano katika Ikulu.

Mkutano huo ulianza saa kumi jioni Jumatano Agosti 21, na kumalizika karibu saa tisa alasiri.

Kila aliyehudhuria alitia mfukoni Sh25,000 kama nauli, viongozi kadhaa waliambia Taifa Leo.

Rais William Ruto, Katibu wa Elimu ya Juu, Dkt Beatrice Inyangala, Katibu wa Masuala ya Ndani Raymond Omollo walihudhuria mkutano huo.

Haya ni kulingana na Makamu wa Rais wa chama cha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kabarak, Evans Serem, ambaye alikuwa mmoja wa waliohudhuria aliandika katika mitandao ya kijamii.

Mkutano huo unajiri siku chache baada ya mkutano wa awali na viongozi wa wanafunzi uliofanyika katika Shule ya Serikali ya Kenya kumalizika kwa taharuki.

Mkutano wa awali, kama ule wa Jumatano, ulihusu mfumo tata wa ufadhili wa elimu ya chuo kikuu ulioanzishwa na serikali.

Viongozi wa wanafunzi waliambia Taifa Leo kwamba mkutano huo ulikuwa wa siri kiasi kwamba makamu chansela wengi hawakujua kuwa wanafunzi wao walikuwa wamealikwa Ikulu.

Duru kadhaa katika mkutano zilisema ni viongozi wa wanafunzi walio na ushawishi tu na wale walio karibu na mamlaka ambao walipokea mwaliko.

Ikulu au Rais William Ruto, ambaye kwa kawaida huchapisha picha baada ya mkutano wa hali ya juu kama huo, hawakuwa wamechapisha maelezo kuhusu mkutano huo wakati wa kwenda mitamboni.

Hata hivyo, picha za baadhi ya viongozi wa wanafunzi walizopiga zimesambazwa mtandaoni.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed aliambia Taifa Leo kwamba mazungumzo yalilenga hali ya elimu ya chuo kikuu na mfumo mpya wa ufadhili.

“Mkutano ulikuwa sehemu ya mfululizo wa mazungumzo na viongozi wa wanafunzi, ambao ni wadau muhimu katika mdahalo kuhusu Hali ya Elimu ya Vyuo Vikuu na mfumo wa ufadhili,” Bw Hussein alieleza. “Ilikubaliwa kuwa siku zijazo, wanafunzi watakuwa na jukumu kubwa katika kutunga sera zinazohusiana na elimu ya chuo kikuu, ikiwa ni pamoja na ufadhili na masuala mengine muhimu.”

Ulikuwa ni mkutano wa wazi ambapo waliohudhuria walitoa malalamishi yao.

Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliozungumza, kulingana na waliohudhuria na kuzungumza na Taifa Leo, aliunga mkono mfumo huo wa ufadhili wenye utata.

Wakati wa mkutano na Rais Ruto, viongozi hao wa wanafunzi walikosoa mfumo huo ambao serikali inatetea.

“Hakuna chochote tulichokubaliana. Tulimwambia wazi kwamba sababu ya kukataa mpango huo ni kuwa unawaadhibu wanafunzi,” Katibu Mkuu wa Chama cha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton, Justice Mutuma alisema.

“Ni mbaya,” Bw Mutuma alieleza. “Kwa mfano, ukiangalia wale waliowekwa katika kundi la kwanza, utagundua kwamba wanatakiwa kulipa Sh9,000 kwa muhula ambazo ni sawa…Lakini mwisho wanapomaliza masomo, watakuwa na mkopo wa zaidi ya Sh1 milioni watakazohitajika kulipa. Serikali inawapa kiasi kidogo cha mkopo lakini mwisho, mkopo wanaolipa ni mkubwa.”

Wizara ya Elimu, kulingana na viongozi wa wanafunzi, “haisikilizi.”

Alipohutubia mkutano huo, Rais alilaumu vyombo vya habari kwa kutangaza habari hasi. Hakuzungumzia mfumo huo wa ufadhili; alielekeza maswali kwa maafisa wa wizara (ya elimu) na kutoka HELB,” mdokezi wetu alisema.

Kufuatia kutoelewana, wasaidizi wa rais walisema kwamba kutakuwa na mkutano mwingine Jumapili.

“Lakini wengi wetu tunatilia shaka na hatutahudhuria,” alisema mmoja wa viongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu aliyehudhuria mkutano huo. “Bado kutakuwa na mgomo kuanzia Septemba 9 kama tulivyomwambia Rais.”

Tayari, Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kimetoa notisi ya mgomo.