Michezo

Mfungaji bora KPL asema anafuata nyayo za Waruru na Makwata

June 4th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Mshambulizi wa Ulinzi Stars Enosh Ochieng ndiye mfungaji bora wa KPL msimu wa 2018-2019.

Enosh alipata tuzo hiyo baada ya kufunga jumla ya magoli matatu katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Mount Kenya FC uwanjani Afraha.

Enosh alifunga goli la kwanza kunako dakika ya tisa mchezoni,na nusura aongeze la pili dakika ya 13 lakini kipa Philip Odhiambo wa Mt Kenya alifanya kazi ya ziada na kuondosha mpira katika eneo la hatari.

Hassan Mohammed karibu afunge goli la kusawazisha kunako dakika ya 20 lakini alipokonywa mpira na Nahashon Thiongo hatua chache kabla ya kufika kwenye lango la Ulinzi.

Oscar Wamalwa aliongeza goli la pili kunako dakika ya 50. Enosh aliongeza goli la tatu dakika ya 51,kabla ya kuongeza la nne dakika ya 57 na lake la 20 msimu huu.

Ulinzi Stars wamemaliza msimu wakiwa wamejizolea jumla ya alama 45 huku wameshikilia nambari nane katika jedwali.

“Imenipa motisha kuwa mchezaji wa tatu kutoka timu ya Ulinzi, kuibuka mfungaji bora tangu michuano ya KPL ianze. Wa kwanza alikuwa Stephen Waruru mwaka wa 2011 aliyefunga mabao 12, kisha John Makwata aliyefunga magoli 15 mnamo 2016,” Enosh akasema.

.Enosh Ochieng wa Ulinzi Stars (kulia) aking’ang’ania mpira na Norman Warunga wa Mt Kenya. Ulinzi stars walishinda 4-0. Picha/Richard Maosi

Enosh alieleza kuwa msimu huu amecheza jumla ya mechi 33,na alikosa mechi moja tu dhidi ya Vihiga United kutokana na jeraha.

Mkufunzi Benjamin Nyangweso alisema Enosh alistahili tuzo hilo kwa sababu amejaliwa kipaji cha kusakata soka mbali,na kuwa mchezaji mwenye bidii na nidhamu.

“Ametoa nafasi nzuri kwa washambulizi wenzake kuiga mfano wake ili kuimarisha ushindani wa kikosi,” Nyangweso alisema.

Kulingana na Enosh kuibuka kuwa mfungaji bora kumempatia motisha hasa baada ya kutajwa kwenye kikosi cha wachezaji 30 wa Harambee Stars, watakaowakilisha Kenya kwenye pambano la CHAN ,Agosti nchini Burundi.

Anasema kocha Sebastein Migne aliona uwezo wake ndipo akamtaja kwenye kikosi kitakachowakilisha Kenya.

“Kuna wachezaji wengi wanaoshiriki michuano ya KPL lakini hawakuitwa kwenye kambi ya timu ya taifa, hii inanipatia fursa ya kujitangaza”akasema.

Aliongezea kuwa hii ni mara yake ya kwanza kujumuishwa kwenye kikosi kitakachowakilisha taifa kwenye mashindano ya CHAN.

Kulingana na Enosh timu nyingi za humu nchini na ukanda wa Afrika Mashariki zinammezea mate ili kupata saini yake,lakini cha msingi ni kuwajibikia michuano iliyo mbele yake kwanza kabla ya kuzungumzia swala la uhamishao.