Michezo

MFUNGAJI BORA: Takwimu mpya zaonyesha ni Wanga na wala sio Enosh Ochieng’

August 23rd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SIKU chache baada ya Enosh Ochieng’ kutangazwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Soka ya Kenya ya msimu 2018-2019 hapo Agosti 19, huenda mshambuliaji huyo akalazimika kurudisha zawadi ya Sh250,000 na runinga ya inchi 49 aliyopokea kutoka kwa kampuni ya vifaa vya kielekroniki ya LG.

Hii ni baada ya kampuni inayoendesha ligi hii (KPL) kutoa takwimu za msimu huo zinazoonyesha kuwa Allan Wanga ndiye aliibuka mfungaji bora.

Kulingana na takwimu mpya kutoka kwa KPL, washambuliaji watatu Wanga (Kakamega Homeboyz), Mganda Umaru Kasumba (Sofapaka) na Ochieng’ (Ulinzi Stars) walimaliza msimu huo kwa mabao 17 kila mmoja. Hata hivyo, Wanga yuko juu ya orodha hiyo ya wafungaji 132 kwa alama 1.18 dhidi ya Kasumba (1.06) na Ochieng’ (0.88).

Mabadiliko haya, KPL inasema, yametokana na kufutiliwa mbali kwa ushindi wa Ulinzi Stars wa mabao 4-0 dhidi ya Mount Kenya United uwanjani Afraha mnamo Juni 2, 2019.

“Matokeo ya mechi hiyo iliyopangwa tena yanafutiliwa mbali,” kampuni hiyo imesema kabla ya kuongeza kuwa Ulinzi bado ilippokea ushindi, lakini wa bwerere wa mabao 3-0 na alama tatu.

Ni kati mechi hiyo ambapo Ochieng’ alifunga mabao matatu yaliyomwezesha kumpiku Wanga na kuwa mfungaji bora kwa kuwa na jumla ya mabao 20.

Pia, Wanga, ambaye alikuwa amekamilisha msimu huo kwa magoli 18, amepokonywa bao moja baada ya Ulinzi kulalamika kuwa aliongezwa bao ambalo kipa Jairus Adira wa AFC Leopards alijifunga mwenyewe.

“Baada ya kuangalia mechi hiyo tena, bao hilo la utata, imeamuliwa kuwa Adira alijifunga na wala si Wanga alifunga bao hilo.

Magoli yapungua

Kwa hivto, idadi ya magoli ya Wanga ya msimu 2018-2019 yanapungua kutoka 18 hadi 17.

Ochieng’ alizawadiwa na LG kama mfungaji bora wa msimu uliopita katika hafla ya kutuza mwanasoka bora wa msimu 2018-2019, ambayo pengine Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF) lilifahamua kutakuwepo na mabadiliko kama haya iliposusia shughuli hiyo.

Haijulikani sasa hatua itakayochukuliwa kurekebisha hali hiyo ya kutoa zawadi, ingawa uamuzi wa KPL sasa unaoneka kumtendea Wanga haki, ambaye baadhi ya mashabiki walihisi walistahili kuwa mfungaji bora wa msimu huo na kudai kuwa mechi kati ya Ulinzi na Mount Kenya United ilipangwa ili kuwezesha Ochieng’ kutwaa taji hilo.

Hakuna mabadiliko yameshuhudiwa kwenye jedwali ambalo lilishuhudia Gor Mahia ikitangazwa mshindo baada ya kuvuna alama 72. Homeboyz ilikamilisha katika nafasi ya saba kwa alama 52 nayo Ulinzi ikaridhika katika nafasi ya 10 kwa alama 45. Vihiga United na Mount Kenya United zilizomaliza ligi hiyo ya klabu 18, zilitemwa.

Msimu mpya unatarajiwa kuanza Agosti 30.