Habari Mseto

Mfungwa aliyetoroka ajirejesha gerezani

March 19th, 2019 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

TAHARUKI ilitanda katika gereza la Manyani, kaunti ya Taita Taveta baada ya mfungwa mmoja kutoroka Jumapili usiku.

Askari jela wa gereza hilo walifanikiwa kumkamata mfungwa huyo baada ya kufanya msako katika eneo hilo la Manyani.

Inadaiwa kuwa mfungwa huyo anayetumikia kifungo cha maisha kwa shtaka la wizi wa mabavu ana upungufu wa akili.

Akithibitisha kisa hicho, msimamizi wa magereza katika kaunti hiyo Bw Nicholas Maswai alisema kuwa mfungwa huyo alitoroka kupitia mtaro wa maji.

Bw Maswai alisema kuwa kabla ya kutoroka kwake alikuwa ametengwa kutokana na hali yake ya kiafya.

“Tulimshika akiwa njiani anarudi gerezani. Tulianza kumsaka punde tu alipotoroka,” akasema.

Bw Maswai alisema kuwa mahabusu huyo vilevile anatumikia kifungo cha kujaribu kutoroka jela mwaka wa 2015.

Alisema ulinzi mkali umewekwa katika kituo hicho ili kuzuia visa kama hivyo.